Kama Taifa, mipango ya maendeleo ya muda mrefu ni muhimu ili kujenga uelewa wa pamoja wa nini kinachohitajika na wapi pa kufika kupitia ukusanyaji wa maoni ya wananchi juu ya dira ya Taifa na Katiba mpya, mchakato utakaowashirikisha kwa upana Wananchi wa makundi mbalimbali katika utoaji wa maoni.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo wakati akifanya mahojiano maalum na Dar24 Media hivi karibuni na kuongeza kuwa hakuna wazo litakaloachwa, ili kuhakikisha kila Mwananchi anaguswa na kulingana na maoni yake.
Amesema, “na hili limegawanyika katika maeneo matatu la kwanza ni wataalam kutumia sampuli ya bahati nasibu kwa kutumia madodoso kwa kuwahoji baadhi ya watu kwa niaba ya wenzao, eneo la pili ni kuyafikia makundi mbalimbali ya Wananchi katika mikoa na ngazi ya tatu ni kuyafikia makundi mbalimbalibya kijamii wakiwemo Wakulima na Wafugaji.”
Prof. Mkumbo ameongeza kuwa, jopo hilo la wataalamu wapatao 22 wenye taaluma mbalimbali litakusanya maoni yote bila kubagua kwamba yepi na sahihi au si sahihi, kisha watachambua kulingana na mahitaji kama ya kiuchumi, elimu, afya nk, kutokana na uhalisia kuwa hakuna Mwananchi aliyefundishwa kutoa maoni bali maelezobyake yatatoa mwanga wa hitaji lake husika.
Hata hivyo, Wataalamu hao wanatabiriwa kukumbana na maoni yanayowiana katika kuandika Katiba mpya, ili kutoa dira ya Taifa linalopaswa kujengwa kwa kipindi kirefu kijacho, ikiwemo maadili ya kitaifa.