Kilimo ni moja ya shughuli ya Mwanadamu ambayo humsaidia kupata mazao kwa ajili ya chakula na mazao mengine kwa ajili ya biashara inayoweza kumuingizia kipato kwa ajili ya maisha yake na kupitia kipato hicho husaidia kukuza uchumi wa nchi yake, ili kujikomboa kiuchumi.

Sekta hiyo ndiyo kiinua uchumi kikubwa kwa mataifa mengi, na kiujumla serikali zinatakiwa zitoe kipaumbele kwa sekta ya kilimo, ili kuepukana na janga la njaa kwani mojawapo ya mahitaji makuu ya mwanadamu ni chakula hivyo kuna umuhimu wa kuongeza zana za kilimo ili watu walime na wapate mazao ya biashara na chakula kwa wingi.

Wakati wa uzinduzi wa maonesho ya Kilimo na Biashara yaliyofaninyika Wilayani Gairo Mkoani Morogoro mapema mwaka huu (2024), Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima alitoa wito kwa Viongozi kuhakikisha wanakuwa na uwelewa kuhusu Kilimo, ili kuwaelimisha Wakulima namna sahihi ya kufanya kilimo cha kisasa.

Malima alisema, ‘hakuna uchawi kwenye kilimo’ hivyo ukimuona mtu amepata mazao mengi ujue amefuata taratibu za kilimo ikiwemo kuweka mbolea, mbegu bora na ushauri wa wataalam wa Kilimo huku Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Jabiri Makame akisema bado wananchi wengi wanalima kilimo cha mazoea na kukosa mazao mengi na kushindwa kujikwamua kiuchumi.

“Serikali inaweza kuleta Umeme, Maji, Barabara na Vituo vya Afya lakini kama tusipoboresha kipato cha Mwananchi mmoja mmoja ni kazi bure, dhamira yetu kila Mwananchi awe na maisha bora, Nyumba nzuri pamoja na kumiliki Bima ya Afya,” alisema Makame.

Kutokana na kauli hizi, ni wazi kuwa Serikali inatakiwa kutoa elimu juu ya kilimo bora kama kitega uchumi ambacho huwasaidia watu kujipatia mazao na kipato cha kuendesha maisha yao binafsi na kuelezwa umuhimu wa kujishughulisha na kilimo cha umwagiliaji na si tu kutegemea mvua pekee.

Kihistoria tunaarifiwa kwamba Watu walianza kulima takriban miaka 10,000 iliyopita, lakini kabla ya hapo waliwinda na kukusanya matunda kwa ajili ya chakula. Hata hivyo, bado kuna vikundi vidogo ambavyo vinaendelea na maisha haya hadi leo, lakini zaidi ya asilimia 99 ya binadamu hupata chakula kutokana na kilimo, hivyo mkulima ni vyema akasaidiwa.

Inaaminika kuwa kilimo kilianza katika sehemu tatu za dunia ambazo watu walitambua mimea yenye lishe kubwa na kupanda mbegu zake, ikiwemo China, Amerika ya Kaskazini na Mashariki ya Kati, lakini Wataalamu hawakubaliani kama kilimo cha Afrika kina asili yake huko Mashariki ya Kati au kama ilianzishwa barani peke yake.

Kitwanga: Tukiamua kubadilika Polisi watabadilika
MAKALA: Utata ndani ya Kiongozi bora, bora Kiongozi