Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye amezungumzia tengua na teuzi zinazofanyika mara kwa mara na kusema kama utaratibu wa kuwapata watu ungekuwa unafanywa vyema na mfumo au Taasisi zinazohusika kuchambua, kuchunguza na kupendekeza majina vyema, Rais hangekuwa na sababu ya kuteua na kutengua.
Sumaye aliyasema hayo katika moja ya mahojiano aliyoyafanya na Dar24 Media jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa Rais hawezi kufahamu watu wote na kwamba hata kama anawafahamu watu hawezi kuteuwa bila kushirikisha mfumo unaohusika, hivyo Rais hana kosa katika teuzi na tenguzi anazozifanya.
Amesema, “ule mfumo kama haufanyi kazi yake vizuri ndiyo haya yanatokea, maana analetewa mtu anaambiwa huyu ndiye anafaa katika nafasi hii anamteua maana yeye hamjui, halafu kesho anakuja mtu mwingine anasema Rais angalia yule uliyemteuwa mambo yake, sasa hapo utaratajia Rais afanye nini?, inabidi atengue lakini kosa ni la wale wanaompelekea mapendekezo.”
Kuhusu eneo ambalo Rais Samia anapaswa kulitilia mkazo kiutendaji, Sumaye amesema angemshauri rais Samia aweke mkazo katika suala la uchumi ambalo litajenga ajira kwa haraka kwani Vijana wengi wamejazana mtaani hivyo badala ya kuangalia uchumi wa muda mrefu usio na matokea ya haraka ni bora kupigania hali iliyopo baada ya uwepo wa changamoto za mdororo wa uchumi Nchini kwa kipindi kilichopita.
“Na kwa bahati nzuri sasa hivi Watanzania wengi ni wasomi, kwahiyo ni lazima kutengeneza njia ambazo zitawabeba Vijana hawa wote kwa haraka, unatafuta Viwanda vile ambavyo vinaajiri watu wengi kwa mara moja, hivyo ndivyo vitakavyoweza kuokoa hili jambo kwa muda mfupi, kwasababu wanapokosa ajira tatizo halipo kwao tu, bali hata kwa wazazi wao,” amesema Sumaye.