Swaum Katambo – Katavi.
Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi imempumzisha majukumu yake Mwalimu Ndikuliyo Mbatenga, anayedaiwa kuwalazimisha Wanafunzi kuzibua vyoo kwa kutumia mikono kama adhabu, pasipo tahadhari ya kiafya.
Hatua hiyo, inakuja baada ya Wananchi wa Mtaa wa Kawalyowa Kata ya Ilembo, kulalamikia kitendo cha Mwalimu huyo anayefundisha Shule ya Sekondari Kawalyowa kuwalazimisha baadhi ya wanafunzi kutoa kitu kilichosababisha choo kuziba, kwa kutumia mikono.
Mwalimu Mbatenga anadaiwa kufanya kitendo hicho kama adhabu kwa Wanafunzi hao aliowatuhumu kula karanga wakati wanavuna shamba la shule.
Crispin Mwanalinze, mmoja wa wazazi wa Wanafunzi waliokumbwa na dhahama hiyo ameeleza kuwa mwanaye alimweleza kuwa kabla ya kulazimishwa kuzibua vyoo, Mwalimu huyo aliwapeleka ofisini na kuwavua nguo kisha kumchapa viboko wakiwa uchi na adhabu hiyo kuendelea siku ya jumatatu kwa kuzibua tundu la choo lililokuwa limeziba, kwa kutumia mikono.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda, Deodatus Kangu amekiri kuwepo kwa tukio hilo ambapo baada ya kupokea taarifa hiyo, alituma timu iliyofanya kikao ambapo Mwalimu alikiri.
Amesema, “baada ya mwalimu kukiri tayari hatua zimechukuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na kumpumzisha majukumu yake na kuunda kamati ndogo ya uchunguzi itakayochunguza matukio yote na baada ya hapo hatua zaidi zitachukuliwa dhidi yake.”
Diwani wa Kata ya Ilembo, Joseph Kang’ombe amesema Mwalimu huyo hashauriki na amekuwa na kauli mbaya kwa Wanafunzi, hivyo ameiomba Serikali kumuondoa katika shule hiyo kwani kitendo alichokifanya ni ukatili na endapo hataondolewa atawahamasisha Wananchi kuandamana kuishinikiza afutwe kazi.