Wananchi wa visiwa vya Comoro sasa wanaweza kuja Tanzania kupata huduma za afya za kibingwa, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa – BMH.
Hayo yamebaijishwa na Balozi anayeenda kuiwakilisha Tanzania katika visiwa hivyo, Said Othman Yakub, ambaye amesema ataitangaza Hospitali ya Benjamin Mkapa nchini Comoro.
Akiongea na uongozi wa BMH, amesema, “Wananchi wa Comoro kwa sasa wanafata huduma za afya za kibingwa Ulaya, sasa wananchi wanaweza kuja BMH kupata huduma hizo.”
Balozi Yakub pia alimtembelea mtoto wa kumi kupandikizwa uloto katika Kitengo cha Upandikizaji Uloto cha Hospitali hiyo.
Aidha, amesema huduma za kibingwa ambazo ataenda kuzitangaza zaidi ni Upandikizaji Uloto kwa watoto wenye siko seli, Upandikizaji wa Figo kwa watu wenye matatizo ya figo na Matibabu ya Watoto.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dkt. Alphonce Chandika, amemshukuru Balozi kwa kuitembelea BMH na kujionea huduma.