Kwa wasiofahamu neno uchaguzi kwa tafsiri halisi ni mchakato wa kumteua mtu kwa nafasi maalumu katika jamii, hasa cheo na majukumu yanayotokana nacho.
Uchaguzi hufanyika kwa nafasi za uongozi au za mamlaka fulani ukifanyika mara nyingi kwa njia ya kupiga kura kwa wenye haki na sifa za kufanya hivyo, kushiriki kuchagua Viongozi wa Serikali za Mitaa, Wabunge na Rais.
Kwa hapa kwetu, kuhusu nani awe Mbunge au kinyume chake, basi sheria, kanuni na taratibu zimeelekeza kwa uwazi kuwa ni jukumu la wadau waliogawanyika maeneo tofauti kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu kama ifuatavyo.
i. Wapiga kura.
Ni watu ambao huletewa majina ya wagombea na Tume ya Uchaguzi, ili wao wawachague au kuamua ni nani wanamtaka awaongoze kwa kipindi kinachoainishwa kwa mujibu wa taratibu.
ii. Vyama Vya Siasa.
Vyenyewe hupendekeza majina ya wagombea na kuyapeleka tume, kwani kwa mfumo wetu huwezi kuwa mwakilishi wa jimbo au Kata Kama hujapendekezwa na Chama chako cha Siasa na pia huwezi kuwa Mbunge wa Viti Maalum iwapo hujapendekezwa na Chama pia.
iii. Tume ya Uchaguzi.
Hii huidhinisha majina ya Wagombea, kuratibu zoezi la kuwapigia Kura waliopendekezwa, kuwatangaza washindi na kupeleka jina kwa Mamlaka husika, ili zoezi la kuwaapisha lifanyike.
iv. Msajili wa Vyama.
Kazi yake ni kusajili, kusimamia na kuvilea vyama, yeye huiambia Tume kwamba vyama vifuatavyo vimefuzu vigezo, hivyo kutoa maelekezo iwapo mgombea ataletwa basi hawana budi kumpitisha kama amekidhi vigezo.
v. Spika wa Bunge.
Spika kazi yake ni kupokea majina ya Wabunge wateule na kuwaapisha, lakini hana uwezo wa kukataa wala kumuingiza Bungeni mtu ambaye hajaidhinishwa na Tume ya Uchaguzi.
Ikumbukwe kuwa, Tume ya Uchaguzi nayo haina uwezo wa kupeleka jina la mtu akaapishwe Bungeni Kama huyo mtu hajaidhinishwa na Chama chake na baadaye kupigiwa kura na Wananchi.
Hata hivyo, Katiba yetu kiupekee imempa Rais nafasi 10 za kuwateuwa Wabunge nje ya utaratibu wa kupigiwa kura, kama ilivyo kwa Wabunge wa Majimbo na wale wa Viti Maalum.
Endapo mtu au watu watafanya kinyume na hapo, hiyo hufahamika kama ni ‘kukanyaga Katiba’ kwani katika mifumo ya uendeshaji nchi, miongoni mwa makosa makubwa ambayo ukiyafanya utasimuliwa vizazi na vizazi ni kukiuka haki za Binadamu na kukanyaga Katiba.
Katiba ni nini?
Katiba ni sheria au kanuni zinazoainisha jinsi ambavyo Nchi, Chama au Shirika linavyopasa kuendesha shuguli zake.
Kuhusu Nchi, ni wazi kuwa katiba ni sheria mama inayoainisha misingi mikuu ya kisiasa na kuonyesha madaraka na majukumu ya Serikali huku ikiainisha haki za msingi za Wananchi.
Hivyo kuenda kinyume na matakwa ya katiba ni kuwakosea wale unaowaongoza na hapo ndipo huwa inatokea migogoro katika mataifa mengi ulimwenguni, hivyo upo umuhimu mkubwa wa viongozi wa Mataifa kuhakikisha wanailinda na kuiheshimu Katiba kwa maslahi ya Taifa na watu wanaowaongoza.