Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii – NSSF, Mwamini Malemi amesisitiza juu ya uboreshaji wa huduma bora kwa Wanachama na kuendelea kuwajengea uwezo wafanyakazi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 52 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NSSF. Malemi pia alisisitiza kuhusu kuongeza kasi ya ukuaji wa Mfuko, kwa kuifikia sekta binafsi na sekta isiyo rasmi ikiwemo kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utendaji kazi.
Alisema, NSSF itaendelea kusimamia maono ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha Watanzania waliopo katika sekta binafsi na sekta isiyo rasmi wanasajiliwa na Mfuko na waajiri kuwasilisha michango stahiki ya wafanyakazi wao kwa wakati.
Lengo la mkutano huo ni kupitia mpango wa mwaka ujao na Bajeti kwa mwaka 2024/25, ikiwa ni ushirikishwaji wa wafanyakazi katika maamuzi ya kiutendaji. Ufunguzi wa mkutano huo umefanyika katika Hoteli ya Malaika Jijini Mwanza.