Kocha Mkuu wa Paris Saint Germain, Luis Enrique amesema anajivunia kuwa na Kylian Mbappe kwenye timu yake na anaelewa uamuzi wa mfungaji huyo bora wa muda wote katika klabu hiyo kuondoka.
Mbappe, ambaye mkataba wake na PSG unafikia kikomo mwishoni mwa msimu huu, alitangaza kuondoka kwenye klabu hiyo kupitia video Ijumaa ikihitimisha miezi kadhaa za uvumi juu ya hatima yake.
Kitendo cha nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ufaransa kutangaza uamuzi wa kuachana na klabu yake hiyo aliyoitumikia kwa kipindi cha miaka saba kinauweka karibu uhamisho wake kuelekea klabu ya Real Madrid.
“Yote ninayoweza kusema ni mazuri ya Mbappe kama mwanasoka na binadamu,” amesema Luis Enrique alipozungumza na waandishi wa habari.
“Naelewa uamuzi wake. Amekuwa hapa kwa miaka saba na kama nguli wa klabu hii. Ametoa kila kitu kwa ajili ya klabu hii na klabu hii pia imempa kila kitu. Namtakia mafanikio mema huko aendako.
“Najivunia kuwa nae kwenye hii timu. Ametusaidia na ni kiongozi mzuri na amefanya hivyo akiwa na tabasamu kwenye sura yake.”
Lakini kumpoteza Mbappe aliyeifungia PSG mabao 255 kwenye mashindano yote na kushinda mataji sita ya Ligi Kuu ya Ufaransa, hakutabadilisha kitu kwenye klabu hiyo, kwa mujibu wa Enrique.
“Haya ni mambo tuliyoyajua kwa muda mrefu jana tu yamewekwa wazi,” amesema kocha huyo wa zamani wa Barcelona.
“Lakini haitabadili kitu chochote kwa muonekano wa ujumla wa klabu yetu. Kila kitu kitabakia kama kilivyokuwa.”
“Bila kujali nani atakuwa hapo au hatakuwa hapa, lengo langu ni kuwa imara zaidi msimu ujao,”
Luis Enrique amesema kutolewa kwenye hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya Borrusia Dortmund bado kunamuumiza na kusema ni muhimu kwa timu hiyo kumaliza msimu kwa kushinda Kombe la Ligi UFaransa watakapokutana na Lyon Mei 25.
“PSG itaendelea kuwa timu kubwa na itakuwa imara zaidi. Tutaleta wachezaji wenye mtazamo mkubwa na wachezaji watakayeitambulisha klabu. Hivyo ndivyo maisha yalivyo,” aliongeza.