Johansen Buberwa – Kagera.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwasa ameahidi kumpatia kiwanja na kumjengea nyumba Bibi wa miaka 61 mwenye wajukuu sita, Catherine Athanael ambaye nyumba yake ilidondoshwa na mafuriko katika mtaa wa Migera uliopo Manispaaa ya Bukoba.
Mwassa ametoa ahadi hiyo wakati akikagua nyumba zilizoathiriwa na mafuriko katika Manispaa ya Bukoba na kusema ofisi yake imeguswa na maisha ya mjane huyo na hivyo atampatia kiwanja na kumjengea nyumba ya vyumba viwili, ili aweze kupata mahali pa kujihifadhi.
Aidha, na amewataka watoto wa bibi huyo kurudi nyumbani ili waweze kulea watoto wao na kuwa serikali iko tayari kuwapatia mitaji ya biashara itakayowasaidia kumudu maisha.
Kwa upande wake Bi Catherine amesema kwa sasa hana pa kuishi na amehifadhiwa na msamaria mwema yeye na wajukuu wake huku akiwa hajui hatima ya maisha yake kwani afya yake inazidi kuzorota na kwamba wajukuu hao sita ni yatima.