Mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 1,774 mwaka 2020/2021 hadi kufikia tani 14,701 mwaka 2022/2023, hatua ambayo imechangiwa na ushirikiano wa kibiashara na mataifa mbalimbali duniani, uliohamasishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa hafla ya uzinduzi na makabidhiano ya Kituo Atamizi cha Ufugaji wa Kibiashara kwa Vijana kilichopo Kongwa mkoani Dodoma, ambacho ni maalum kwa ajili ya unenepeshaji wa mbuzi kilichogharimu Shilingi Bilioni 1.6.

Amesema, “Masoko ya nyama yameendelea kuongezeka na kuzifikia nchi 12 ambazo ni Bahrain, Comoro, Hong Kong, Jordan, Kenya, Kuwait, Oman, Qatar, Rwanda, Saudi Arabia, UAE na Vietnam.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Ameongeza kuwa, Nyama ya Mbuzi imeendelea kuongoza katika mauzo ya nyama nje ya nchi ambapo imechangia asilimia 70.1 ya mauzo yote na kutoa wito kwa Vijana kuitumia fursa ya uwepo wa kituo hicho kwa manufaa yao binafsi na manufaa ya taifa kwa ujumla.

“Lengo la mradi unaokabidhiwa leo ni kuwapatia vijana ujuzi kwa vitendo ikiwemo elimu ya ujenzi wa mabanda, ulishaji, matibabu na usimamizi wa mradi wa ufugaji mbuzi lakini pia kutoa mafunzo ya biashara ili wawe wajasiriamali na waweze kuendeleza biashara ya unenepeshaji mbuzi,” amesema Majaliwa.

Kai Havertz: nitaishangilia Tottenham Hotspurs
Failuna kukosa michuano ya Olimpiki 2024