Mwanariadha wa Kimataifa wa Marathoni kwa Wanawake, Failuna Abdi hatashiriki Michezo ya 33 ya Olimpiki itakayofanyika Paris nchini Ufaransa mwaka huu baada ya kushindwa kufikia viwango.
Failuna aliwahi kuiwakilisha nchi katika mashindano mbalimbali makubwa, kama angefuzu angeungana na Wanariadha wengine wa kike, Jackline Sakilu na Magdalena Shauri ambao tayari walishafuzu kupitia mashindano mbalimbali.
Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania ‘RT’, Jackson Ndaweka amesema Failuna alishiriki Hannover Marathon nchini Ujerumani hivi karibuni, lakini alishindwa kufikia muda wa kufuzu.
Katika mbio hizo, Failuna alimaliza wa tano kwa kutumia saa 2:27:36 wakati muda wa kufuzu Marathoni kwa wanawake katika Michezo ya Olimpiki ni saa 2:26:54.
Mbali na Jackline na Madgalena, wanariadha wengine waliofuzu kushiriki Olimpiki mbio za Marathoni ni Alphoae Simbu, ambao kwa sasa wanaendelea na maandalizi ya michezo hiyo.
Ndaweka amesema kwa upande wa Marathoni, Mashindano ya kufuzu yameshamalizika na sasa yamebaki yale ya kufuzu kwa mbio fupi ambayo yatafungwa mwishoni mwa mwezi huu na Tanzania inatarajia kupeleka Wanariadha kadhaa ili kusaka viwango.