Wakati jana Jumatatu (Mei 13) Young Africans ikitangaza ubingwa wake wa tatu mfululizo baada ya kuifunga Mtibwa Sugar mabao 3-1, Kaimu Kocha wa Simba SC, Juma Mgunda, amesema timu hiyo bado ina nafasi ya kumaliza ligi nyuma ya mabingwa hao mara tatu mfululizo licha ya sare waliyoipata juzi Jumapili (Mei 12) dhidi ya Kagera Sugar.

Simba SC ilikuwa na nafasi ya kupanda mpaka nafasi ya pili kama ingefanikiwa kupata ushindi kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba na kuambulia sare ya bao 1-1.

Akizungumza baada ya kurejea jijini Dar es salaam Mgunda amesema licha ya sare hiyo dhidi ya Kagera Sugar, bado hawajakata tamaa kumaliza katika nafasi hiyo na kukata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu ujao 2024/25.

“Bado hatujamaliza michezo yote, tulipambana kwenye mchezo dhidi ya Kagera lakini bahati haikuwa kwetu, tunajipanga kwa ajili ya mchezo ujao, kwangu mimi bado haijaisha, bado tuna nafasi ya kumaliza kwenye nafasi ya pili, kikubwa tunatakiwa kufanyia kazi mapungufu tuliyaona ili michezo iliyobaki tupate alama tatu,” amesema Mgunda.

Aidha, amesema wachezaji wake wanapambana sana uwanjani kwa ajili ya kupata alama tatu lakini wamekuwa wakikosa bahati ya kuondoka na ushindi kwenye baadhi ya michezo yao.

“Tutaendelea kupambana, nimewaambia wachezaji wangu wasikate tamaa, waendelee kupambana na kuweka mkazo kwenye michezo yote iliyobakia, hatutaki kuangalia matokea ya timu nyingine, tupambane sisi kushinda michezo yote, naamini tunaweza kufanya vizuri kwenye mechi zote zilizobakia,” amesema Mgunda.

Matokeo ya juzi Jumapili (Mei 12) yameifanya Simba SC kufikisha pointi 57 pointi tatu nyuma ya Azam FC inayoshika nafasi ya pili lakini wakiwa wamecheza mchezo mmoja zaidi ya Simba SC inayoshika nafasi ya tatu.

Mchezo unaofuata, Simba SC itasafiri mpaka Dodoma kucheza na Dodoma Jiiji FC Mei 17 huo utakuwa mchezo wake wa 17.

Wizara ya Habari, USCAF watekeleza mradi wa mnara
Kai Havertz: nitaishangilia Tottenham Hotspurs