Mshambulaiji kutoka nchini Ufaransa Kylian Mbappe atalazimika kupunguza sehemu kubwa ya mshahara wake ili kufanikisha safari ya kutua kwa Mabingwa wa Soka nchini Hispania Real Madrid.
Mshambuliaji huyo wa Paris Saint-Germain aliweka wazi kwamba ataachana na timu hiyo yenye maskani yake Parc des Princes mwishoni mwa msimu huu wakati mkataba wake utakapofika ukomo.
Awali kulikuwa na imani kwamba huenda Mbappe angesaini dili jipya kama alivyofanya mwaka 2022 alipoamua dakika za mwisho, lakini safari hii mambo ni tofauti baada ya mkali huyo wa Les Bleus kufichua kwamba hataongeza mkataba kwenye kikosi hicho, akidai anahitaji changamoto mpya.
Na kinachoelezwa ni kwamba baada ya kutangaza ataachana na PSG, Mshambuliaji huyo sasa anahusishwa na mpango wa kwenda kujiunga na Real Madrid wakati dirisha la usajili wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa.
Kwenye kikosi cha PSG, Mbappe aliripotiwa kulipwa Pauni 64.6 milioni kwa mwaka, pamoja na bonasi ya Pauni 25.8 milioni kutokana na kubaki kwenye timu hiyo hadi mwisho wa msimu wake.
Lakini, sasa atakapokwenda kujiunga na miamba hiyo ya Los Blancos, Mshambuliaji huyo wa zamani wa AS Monaco, atasaini mkataba wa miaka mitano na kulipwa mshahara wa Pauni 12.9 milioni kwa mwaka baada ya makato ya kodi.
Lakini, atalipwa Pauni 129.2 milioni kama ada yake ya usajili, ambayo itakuwa ikilipwa kidogo kidogo katika kipindi cha miaka mitano ya mkataba wake huko Bernabeu.