Uongozi wa Azam FC umedhamiria kwa dhati kumrudisha aliyekuwa Mlinda Lango namba moja wa kikosi hicho, Aishi Manula baada ya msimu huu kufikia tamati.

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zinaeleza kwamba viongozi wanataka kumrejesha nyota huyo aliyeondoka ndani ya kikosi hicho Agosti 9, 2017 huku akiwa ni moja ya makipa bora nchini kutokana na kiwango chake anachokionyesha.

Hesabu hizo zinakuja baada ya Azam FC kutaka kuwaondoa makipa wawili waliopo Mcomoro, Ali Ahamada anayelipwa kiasi kikubwa cha fedha na Mghana, Abdulai Iddrisu ambaye pia inaelezwa hana uhusiano mzuri kikosini humo na Kocha, Youssouph Dabo.

Ahamada na Iddrisu ambao wote kwa sasa ni majeruhi inaelezwa huenda wakatolewa ili kupisha usajili wa Manula ili aende kusaidiana na Mlinda Lango Mohamed Mustafa aliyepo kwa mkopo akitokea Al-Merrikh ya Sedan kwani viongozi wanahitaji kumsajili moja kwa moja.

Manula alihitajika mwanzoni tu kujiunga na timu yake ya zamani ingawa dili hilo lilishindikana kwa kile ambacho Simba SC ilihitaji kubadilishana na kiungo nyota wa kikosi hicho, Sospeter Bajana jambo ambalo viongozi wa Azam FC hawakukubaliana nalo.

Hata hivyo taarifa zinaeleza kuwa viongozi wa Azam FC wameanza kumfuatilia Manula ili kutaka kujua ukubwa wa jeraha la oparesheni ya nyonga aliyofanyiwa huku madaktari wa timu hiyo wakielezwa kumtibia ili apone haraka.

“Ni kweli kumekuwa na mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Simba SC na viongozi wa Azam FC wakihitaji kumrudisha tena ndani ya timu hiyo, jambo nzuri ni kwamba mchezaji mwenyewe ameonyesha nia ya kuondoka mwisho wa msimu,” kimesema chanzo hicho.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin Popat’ alipotafutwa kuzungumzia suala hilo amesema, jambo lolote ambalo linawahusu kama klabu wana utaratibu wao mzuri wa kulitolea taarifa kupitia vyanzo vyao mbalimbali ikiwa kuna ulazima.

Taarifa zote huwa tunaziweka katika mitandao yetu rasmi ya klabu hivyo nisingependa kulizungumzia hilo kwa sasa, kwa sababu ni tetesi kama zilivyokuwa nyingine, mashabiki zetu watapata ukweli wowote pale ambapo tutakamilisha kila kitu.”

Kwa upande wa Meneja  Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema suala mchezaji kubaki au kuondoka litafahamika baada ya msimu kuisha ingawa wao kama viongozi lengo lao ni kubaki na wachezaji wao wote waliokuwa bora kikosini humo.

Manula ameonyesha uwezo mkubwa hadi kuitwa ‘Tanzania One’ ambapo sio bahati mbaya kwani tangu ajiunge na Simba SC ametwaa mataji mengi yakiwemo ya Ligi Kuu Bara kwa mara nne mfululizo kuanzia msimu wa 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021.

Mbali na mataji hayo ila amechukua tuzo nyingi binafsi huku akikiwezesha kikosi hicho kutinga hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa mara tano kati ya sita mfululizo huku mara moja ikiwa ni la Kombe la Shirikisho la Barani Afrika.

Mlinda Lango huyo ambaye amekuwa panga pangua ndani ya Simba SC, kwa sasa amekuwa na msimu mbovu kutokana na kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara huku akiachia nafasi kwa Mmorocco Ayoub Lakred anayeonyesha kiwango bora tangu alipotua akitokea FAR Rabat ya nchini humo.

Tayari Azam FC imeanza usajili mapema kwa ajili ya msimu ujao.

Manyara: Mtui awaita wasiolipa kodi ya Ardhi
Mbappe kujipunja mshahara Real Madrid