Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC, Juma Mgunda amesema kuwa maandalizi ya kuikabili Dodomna Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Mei 16 wameyaanza jana mjini Bukoba baada ya kutoka sare ya 1-1 na Kagera Sugar.
Mgunda ameyasema hayo, huku kikosi chake kikiwa katika maandalizi ya mchezo dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma keshokutwa Alhamisi (Mei 16).
Kocha huyo hiyo ni mechi yake ya pili kutoka sare tangu achukue mikoba kutoka kwa aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha aliyeondoka kwenda kumuuguza mkewe nchini Algeria.
Amesema kutokana na umuhimnu wa mchezo huo ndio maana kikosi chake kilianza mazoezi jana Jumatatu (Mei 13) asubuhi kwenye Uwanja wa Kaitaba na mchana kilianza safari kurudi Dar es salaam kuendelea na maandalizi ya mchezo huo.
Akizungumzia mchezo dhidi ya Kagera Sugar, Mgunda amesema ulikuwa mgumu kutokana na kila timu kuwa na malengo yanayofanana ya kuzitaka pointi tatu kwa nguvu zote.
Amekiri kuwa wachezaji wake walitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini pia walikosa mabao mengi kwa baadhi yao kukosa umakini walipofika katika eneo la hatari.
Amesema kuwa wameanza kufanyia kazi kasoro na mapungufu yote yaliyojitokeza katika mchezo wa juzi Jumapili (Mei 12) ili kuhakikisha wachezaji wake hawarudii makosa hayo katika mechi zijazo.
Sare hiyo imezidi kuiweka Simba Sc katika nafasi ngumu ya kumaliza ya pili baada ya Azam FC kuifunga KMC kwa mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex na kuendelea kujikita katika nafasi ya pili.