Wakati timu zikiwa sokoni kusaka majembe kwa ajili ya msimu ujao, miongoni mwa majina yaliyopo mezani kwa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans ni jina la kipa wa Singida Fountain Gate, Beno Kakolanya.

Hilo limejiri baada ya uongozi wa Klabu hiyo kufikia uamuzi wa mwisho wa kuachana na Metacha Mnata aliyewahi kuichezea Singida Big Stars.

Inadaiwa kuwa miongoni mwa sababu zilizosababisha kuondolewa kwa kipa huyo ni pamoja utovu wa nidhamu unaojirudia mara kwa mnara.

Hata hivyo, majina yaliyopo mezani kwa sasa ni pamoja na la kipa wa Tanzania Prisons, Amos Yona na Kakolanya ambapo wote wanajadiliwa.

Taarifa za ndani kutoka Young Africans zinaeleza kwamba mabosi kwa sasa wamegawanyiká huku upande mwingine ukionyesha kumhitaji Beno na wengine wakimkataa kutokana na kinachodaiwa kuwa utovu wa nidhamu.

“Bado tuko kwenye mazungumzo ili tufikie muafaka wa kuchagua nani tutakaemsajili ili kushika nafasi ya Metacha kwani hatutakuwa naye msimu ujao. Kipa wa Prisons (Amos) hana shida ila kinachomuangusha ni uzoefu wa mechi za kimataifa ambapo hapo ndipo Beno anampiga bao, kwani ana ujuzi wa muda mrefu linapokuja suala la mechi hizo”

Tunahitaji kipa mzawa ili kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni kwani tuna mpango wa kuendelea kusajili na kipa namba moja ni mgeni, hivyo tutawaongeza kwenye maeneo mengine, ila kwa hapa lazima apatikane mrithi wa Metacha ambae ni lazima awe mzawa.”

Beno ambaye amewahi kuichezea Young Africans kabla ya kwenda Simba SC ana uzoefu wa kucheza michuano ya kimataifa, huku msimu huu aliopo Singida Fountain Gate amecheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Hata hivyo, kipa huyo ambaye kwa sasa yupo nje ya timu hiyo kutokana na kinachodaiwa kuwa matatizo na uongozi msimu huu amecheza mechi 10 za ligi na kuruhusu mabao 14, ilhali Amos akicheza mechi 25 na kuruhusu mabao 26, akiwa hana rekodi ya kutocheza mechi kimataifa.

Neymar awaahidi furaha mashabiki Al Hilal
Dkt. Yonaz ataka ufanisi utendaji wa shughuli za Serikali