Kocha Mkuu wa Azam FC Youssouph Dabo amesema timu yake bado ina kazi kubwa ya kufanya kushinda mechi zake tatu zilizobaki katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2023/24.

Dabo ametoa kauli hiyo baada ya timu hiyo kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya KMC katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam.

Wakati Young Africans ikiwa kileleni mwa ligi hiyo, vita kubwa ipo nafasi ya pili na tatu kati ya Azam FC yenye pointi 60 katika mechi 27 na Simba SC iliyovuna pointi 57 katika michezo 26.

Katika ligi hiyo, Azam FC inayosaka nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu ujao 2024/25, imebakiwa na mechi dhidi ya JKT Tanzania, Kagera Sugar na Geita Gold.

Dabo amesema mechi za mwishoni mwa msimu mara nyingi huwa ngumu, hivyo ataendelea kutoa mbinu mpya kwa kikosi chake kupata ushindi.

Kocha huyo Msenegali, amesema lengo lake kubwa ni kuiona timu yake ikimaliza katika nafasi za juu, hivyo watapambana kushinda kila mechi.

“Bado nina kazi kubwa ya kufanya katika mechi zangu tatu zilizobakia, nahitaji kupata ushindi katika mechi hizo ili kufanikisha hilo, natakiwa kuongeza nguvu kubwa kwa wachezaji kwa kuwaongezea mbinu zaidi,” amesema Dabo

Simba SC kuibomoa Coastal Union
Neymar awaahidi furaha mashabiki Al Hilal