Mshambuliaji wa Kagera Sugar Obrey Chirwa ameeleza maana ya shangilia ya bao alilowafunga Simba SC akisema anawarushia kijembe kuwajibu ambao walimkataa kwa kumuona mshambuliaji mzee.
Kwenye mchezo wa juzi Jumapili (Mei 12) Kagera ikiwa nyumbani Chirwa aliisawazishia Kagera bao wakati timu yake ikiwa nyuma na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa sare, ambapo baada ya kufunga alikwenda kushangilia kwenye kibendera akishika mti huo na kutembea mithili ya babu mzee mwenye mkongojo.
Akizungumza mjini Bukoba Chirwa raia wa Zambia amesema shangilia ile ilikuwa ujumbe kwa timu kubwa hapa nchini ambazo ziliwahi kumwacha na kumkataa kwa madai amezeeka.
Chirwa amesema mbali na kuifunga Simba SC alipanga pia kuzifunga Young Africans ambao walinusurika kidogo sambamba na Azam FC ambazo amejipanga msimu ujao.
“Hizo timu ziliniacha baadhi na nyingine zikadai mimi mzee lakini nilisema kila nitakapokutana nao nataka kuwafunga ili wajue mimi sio mzee na nikabahatika kuwafunga Simba SC,” amesema Chirwa ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Young Africans, Azam FC na Namungo FC.
Young Africans wana bahati sana mechi ya kwanza nilishawafunga waamuzi wakawabeba, nikawakosa mechi ya pili kidogo na bado Azam hapa Tanzania kuna dharau sana watu wakikuzoea.”
“Mimi bado ni mshambuliaji mwenye nguvu nyingi lakini wao wanakuona mzee dawa yao ni kuwafunga na kuwajibu kama vile ili waheshimu wachezaji.” Amesema Chirwa ambaye amefunga mabao matano msimu huu