Uongozi wa Simba SC umeanza mchakato wa kuhakikisha unambakisha Mlinda Lango wake chaguo la kwanza Ayoub Lakred, kwa kumpa mkataba mpya wa miaka miwili ya kuendelea kuitumikia klabu hiyo ya Msimbazi.

Mbali na Lakred, taarifa kutoka Simba SC zinasema mabosi wa timu hiyo pia wameweka wazi hakuna ofa rasmi kutoka katika timu yoyote kwa ajili ya kuhitaji huduma ya beki wao Mkongomani, Henock Inonga.

Lakred, nyota raia wa Morocco, alisaini mkataba wa mwaka mmoja ambao unafikia tamati mwisho wa msimu huu.

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es salaam zinasema viongozi wamekamilisha mazungumzo na kipa huyo ataendelea kusalia Msimbazi baada ya kukubali kuongeza mkataba wa miaka miwili.

“Mambo yameenda vizuri kwa upande wa Lakred, viongozi wamefanya mazungumzo naye na ameridhia kubakia Simba SC, atasaini mkataba mpya wa miaka miwili wa kuitumikia klabu yetu,” kimesema chanzo hicho

Kuhusu Inonga, chanzo hicho kimesema bado beki huyo ataendelea kusalia kwa Wekundu hao wa Msimbazi kwa sababu hakuna ofa iliyopelekwa ikihitaji huduma ya Mkongomani huyo.

“Kuna baadhi ya wachezaji ambao mikataba ilifikia tamati wameongezewa, akiwamo Kibu Dennis na Israel Mwenda tayari wameshasaini mkataba wa miaka miwili kila mmoja ili kuendelea kusalia ndani ya Simba SC.

Kuhusu Chama (Clatous), bado amewekewa ofa mezani jukumu lililobakia ni mchezaji mwenyewe kama atasaini au kama akiona haina maslahi kwake amepewa baraka zote za kwenda kupata changamoto nyingine huko aendako. Kiliongeza chanzo hicho

Kilisema pia usajili mpya wamekamilisha na kuwapa mkataba wa miaka miwili ni beki wa Coastal Union, Lameck Lawi huku safari ya kwaheri ikinukia kwa kiungo mshambuliaji kutoka Burundi Saido Ntibazonkiza.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amekiri kufanya mazungumzo na baadhi ya wachezaji waliomaliza mkataba akiwamo Lakred.

“Kuhusu Wachezaji waliomaliza mikataba yao, tunaendelea na mazungumzo ili kuhakikisha tunawabakiza, suala la kocha mchakato unaendelea kwa kufuata mapendekezo yetu ni aina gani ya kocha tunayemhitaji,” amesema Ahmed.

Simba SC kwa sasa iko chini ya Juma Mgunda baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha, kurejea kwao kutokana na matatizo ya kifamilia.

Utekelezaji wa sheria: Ndejembi aipa somo OSHA
Udhibiti wa Ujangili: Rais Samia, Wananchi watajwa