Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa anatarajia kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utakaofanyika Julai 10, 2024 Mkoani Kigoma ambapo uboreshaji utaanza katika mkoa huo kisha kuendelea Katavi, Rukwa na Tabora.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Zanzibar hii leo Mei, 2024 Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele amesema kuwa zoezi hilo litakapokamilika Daftari la Kudumu linatarajiwa kuwa na wapiga kura 34,746,638.

Amesema, “kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Daftari linatarajiwa kuwa na wapiga kura 34,746,638 kutoka 29,754,699 ya mwaka 2020 hili ni ongezeko la wapiga kura wapya 5,586,433 sawa na asilimia 18.7.”

Ameongeza kuwa katika zoezi hilo wapiga kura 4,369,531 wanatarajiwa kuboresha taarifa zao na wapiga kura 594,494 wataondolewa katika Daftari kwa kupoteza sifa za kuwa wapiga kura.

Kuhusu idadi ya vituo, Jaji Mwambegele amesema Tume ilifanya uhakiki wa vituo vya kuandikishia wapiga kura mwaka 2023 ambapo baada ya zoezi hilo iliamuliwa kuwa vituo vya kupigia kura vitakavyotumika kwenye uboreshaji wa Daftari ni 40,126.

“Kabla ya uhakiki huo wa vituo, kulikuwa na vituo 37,814 ambavyo vilitumika kuandikisha wapiga kura mwaka 2019/2020. Baada ya zoezi hilo la uhakiki, jumla ya vituo 40,126 vitatumika kwenye zoezi la uboreshaji wa Daftari mwaka 2024/2025 ambapo kati ya vituo hivyo, 39,709 ni vya Tanzania Bara na vituo 417 ni vya Zanzibar,” amesema Jaji Mwambegele.

Waajiri wasiowasilisha michango ya Wafanyakazi NSSF waonywa
Mateso: Rais, wanawe wawili wagoma kula