Johansen Buberwa – Kagera.
Wadau wa kundi la Whatsapp la Bukoba mjini mpya kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Bukoba mjini Adv. Stephen Byabato wametembelea na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa wahanga wa mafuriko yaliyotokea usiku wa kuamkia Mei 9, 2024 katika kata saba za Manispaa ya Bukoba.
Wadau hao, wamefika katika kata hizo ambazo zimeathiriwa na mafuriko hayo na kutoa vitu mbalimbali ikiwemo Mchele, Unga, Mafuta, Sabuni, Maharage na nguo kwa ajili ya kuwasaidia wahanga hao kupata mahitaji hayo muhimu ambapo kwa kila Kata kaya 15 zimepatiwa msaada huo.
Baadhi ya wadau wa group hilo Jamila Emily, Erick Bashabi, Sharifa Karwani, Asimwe na Husna kwa nyakati tofauti wamesema waliopata mafuriko wanahitaji msaada kutoka kwa wadau mbalimbali, hivyo kwa umoja wao waliona ni vyema kuungana kwa pamoja kuchangishana kama wana group ili kuwasaidia.
Kwa upande wake katibu wa Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Injinia Pasaka Bakari amesema kuwa baada ya mafuriko kutokea, ofisi ya mbunge ilifika kwa wahanga katika kata zote 7 zilizoathirika, ili kuona athari na amewashukuru wadau mbalimbali wanaoendelea kuwasaidia wahanga na kuwaomba wengine kuendelea kujitokeza.
Amesema, Mbunge Byabato ataendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuona namna ya kuwasaidia waanga wa mafuriko.
Kwa upande wake Afisa Tawala Wilaya ya Bukoba mjini akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Ajesy Katumwa amewashukuru wadau hao kwa kuona umuhimu wa kutoa misaada hiyo.
Nao baadi ya Wananchi waliopatiwa msaada huo wameshukuru wadau hao na Mbunge wa Jimbo la Bukoba mjini kwa msaada walioutoa.