Tatizo la Wanyamapori kugongwa na magari barabarani na kupelekea wengi wao kufa, limewakutanisha Wadau wa masuala ya Utalii Wilayani Longido Mkoani Arusha, ili waweze kujadili namna bora ya kupata ufumbuzi wa kukabiliana na tatizo hilo tatizo hilo linaloathiri ikolojia ya Wanyama.
Katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Shirika la OIKOS Afrika Mashariki, Mary Birdi amesema kupitia utafiti walioufanya
walibaini kuwa Wanyamapori wengi wanakufa kwa kugongwa na magari barabarani hasa ile ya Arusha kuelekea Namanga.
Amesema wadau mbalimbali kutoka Serikalini na Sekta binafsi wameona ipo haja ya kujadiliana na kuweka mikakati ya pamoja ya na kwamba kupitia semina hiyo ya siku tatu wana imani watakuja na mikakati ya pamoja ya nini kifanyike ili kunusuru ama kupunguza madhara zaidi kwa Wanyamapori hao.
Awali, Afisa Wanyamapori Mkuu toka Wizara ya Maliasili na Utalii, Issack Ngowi amesema Viongozi Wakuu wa Kitaifa wamekua wakionesha juhudi za kuutangaza utalii, hivyo na wao watahakikisha wanawaepusha Wanyama hao na vitendo vya kihalifu ikiwemo ujangili.
Naye Mkuu wa Polisi Wilaya ya Longido, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Leah Ncheyeki amesema kwa kushirikia na wadau wengine watafunga kamera za usalama barabara yote ya Namanga Arusha kwa ajili ya kufuatilia mienendo ya uendeshaji wa madereva katika barabara hiyo.
Kwa upande Mkuu wa Ikolojia ya Wanyamapori Kanda ya Longido – Ziwa Natron Bwana Augustino Ngimilanga amesema
ili kuhakikisha wanalinda Wanyama hao, watatoa elimu kwa wananchi hasa madereva wa magari juu ya madhara ya
kugonga wanyama lakini pia kuwaeleza faida ipatikanayo na wanyama hao kupitia utalii.
Baadhi ya madereva mbali na kushukuru elimu waliyoipata, pia wamekiri kwa kiasi kikubwa wao kuwa sababiu ya vifo vingi vya wanyama kwa kutozingatia sheria za usalama barabarani, huku wakitoa wito kwa madereva wenzao kuwa makini na kutaka TANROAD kufyeka majani marefu pembezoni mwa barabara kwakua yanachangia vifo hivyo.