Serikali imetoa Shilingi Milioni 10 kwa Chama cha Mchezo wa Pete (Netiboli) Tanzania ‘CHANETA’ ili kuendesha mashindano ya Klabu Bingwa Afrika yanayoendelea kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema Serikali imetoa fedha hizo ili kuona timu ya Tanzania inafanya vizuri na kulibakisha kombe nyumbani.

“Fedha tutakazowakabidhi tunataka kuona zinazaa matunda katika mashindano hayo sitawaelewa nikiona hamfanyi vizuri, ugomvi wenu na mimi bado haujaisha kwa sababu bado haujafika ninapotaka ufike,” amesema.

Msigwa amesema awali mchezo huo uliyumba kutokana na migogoro iliyokuwepo ndani ya chama hicho na kudai anafarijika kuona uongozi unapambana kuhakikisha mchezo huo unafika mbali zaidi.

“Mwakani nataka nione timu zinaongezeka zaidi pamoja na kuandaa mashindano ya ndani yatakayotufanya tuonekane tumekua kupitia mchezo huu kama ilivyo nchi ya Uganda,” amesema Katibu huyo.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa CHANETA, Dk Devota Marwa amesema amefurahi kusikia kauli hiyo kutoka kwa kiongozi wa Serikali na kuahidi kupambana zaidi ili mchezo huo ufike mbali.

“Nimefarijika baada ya Katibu kuonesha moyo wa kutusaidia fedha hizo ninaahidi kufanya kila linalowezekana ili kuukuza mchezo huu ambao utasaidia wachezaji kupata ajira nje ya nchi, vilevile hujenga afya,” amesema Marwa.

Mashindano hayo ambayo yanatarajiwa kumalizika Mei 18, mwaka huu yameshirikisha timu 12 kutoka nchi za Uganda, Kenya pamoja na visiwani Zanzibar.

Dabo hataki maskhara 2023/24
Msako wa Marouf Tchakei waanza Msimbazi