Kongo zamani ikifahamika kama Zaire, asili ya jina lake ilizaliwa katika Lugha ya Kikongo ambayo ni ya watu wa Kabila la Wakongo, kwasasa ikifahamika kama Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Neno Kongo linatokana na na neno la “Ngo” jina la kiasili kwa watu wa Kongo lenye maana ya Chui na ambalo lilizaa jina la Ufalme wa Kongo (Ufalme wa Chui) au (Royaume Kongo), ambao ulikuja kuwa Congo nyakati za sasa au waweza kusema “Utawala wa milki ya Chui”.
Katikati ya historia ya maisha ya Wakongo (sasa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo), Chui ni ishara nyeti na nembo maalum katika historia ya makabila mengi yanaoiunda nchi hiyo ambapo kitaifa, ni kitambulisho kinachomaanisha nguvu, kujiamini na ushindi.
Inaarifiwa kuwa zamani likitokea tatizo kubwa kama uvamizi wa maadui, wanajamii wote walikuwa wakikimbilia katika maeneo wanapoishi Chui, ili kupata ulinzi wa wanyama hao ambao nao hawakuwa wao bali yule ambaye alikuwa ni adui pekee.
“Tuele ku Ngo” waliambizana watu hao wakimaanisha “Twende kwa Chui” (kwa lugha yao). Kwa hivyo maneno mafupi twaweza yaweka kwamba ni “ku Ngo” na kama ujuavyo katika kutohoa au kupata urahisi ndiyo iliyozaa jina Kongo.
Au tuiweke hivi, limezaliwa kutoka kwa kuyaunganisha maneno mawili ambayo ni “Ko = Kwa” na “Ngo = Chui” likawa neno “Ko-Ngo” yaani “Kwa Chui” (Nyumbani kwa chui = (Milki ya Chui) na hata katika kabila la Kasai, wapishi wakubwa wanaitwa “mukalenga wa nkashama” ambayo ina maana “chui mama” au “tumbo la chui”.
Kiongozi wa Kabila la Wakongo katika asili, ni mnyama Chui, na ndio mana kila kiongozi wa Jamii aliyekuwa akiteuliwa kuliongoza kabila hili, alikuwa akipatikwa jina la “Chui” ambapo katika Lugha ya Kikongo ni “Ngoì” yaani jina la mtu mwenye sifa za kuwa mfalme ambaye pia alikuwa na majukumu magumu yakuilinda Jamii dhidi ya uvamizi wowote.
Chui amekuwa ishara muhimu na ya kijadi iliyoachwa na mababu Nchini Kongo, kiuhalisia akiwa ni mnyama mwindaji anayewinda kimyakimya ingawa ni mdogo kuliko wanyama wote wa jamii ya Panthera, anayeweza kuwinda mnyama mkubwa kutokana na kuwa na fuvu kubwa lenye taya zenye nguvu. Anafanana na paka lakini yeye mwili wake ni mrefu zaidi na miguu yake ni mirefu.