Jumla ya kilogramu milioni 1.96 za dawa za kulevya zimekamatwa mwaka 2023 kutokana na jitihada za Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya – DCEA, kwa ushirikiano wa vyombo vingine vya dola.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama ameyasema hayo mbele ya Vyombo vya Habari wakati akitoa taarifa ya Hali ya dawa za Kulevya 2023 nq kudai kuwa katika ukamataji huo, watuhumiwa 10,522 kati yao wanaume 9,701 na wanawake 821 walikamatwa.
Amesema, “Dawa za kulevya zilizokamatwa ni heroin kilogramu 1,314.28, cocaine kilogramu 3.04, na methamphetamine kilogramu 2,410.82. Nyingine ni bangi kilogramu 1,758,453.58, mirungi kilogramu 202,737.51, skanka kilogramu 423.54 na dawa tiba zenye asili ya kulevya gramu 1,956.9 na mililita 61,672.”
“Takwimu za mwaka 2023 zinaonyesha mafanikio makubwa, kwani kiasi cha dawa za kulevya kilichokamatwa ni kiasi kikubwa kuliko kiasi kilichowahi kukamatwa wakati mwingine wowote nchini.
Kiasi hiki ni karibu mara tatu ya kile kilichokamatwa kuanzia mwaka 2012 hadi 2022, ikiwa ni ishara ya dhamira ya dhati na utashi wa kisiasa wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupambana na janga hili” amesema Mhagama.
Aidha, amesema Serikali imepanua huduma za tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya ambapo hadi kufikia mwezi Disemba 2023, vituo vya tiba saidizi na unasihi kwa waraibu wa dawa za kulevya (MAT Clinics) vilivyohudumia waraibu 15,912 vilifikia 16, na nyumba za upataji nafuu (sober houses) 56 zilizohudumia waraibu 3,488. Pia, jumla ya waraibu 903,062 wa dawa za kulevya na vilevi vingine walipata huduma katika hospitali za wilaya, mikoa na rufaa nchini.
Waziri Jenista amesema, Serikali imeanza ujenzi wa kituo cha Taifa cha Utengamao kwa ajili ya kuwahudumia waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu.
“Kituo hiki kitajengwa katika eneo la Itega Jijini Dodoma na kitasaidia kuwajengea uwezo waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu ili waweze kujikimu kimaisha na kuepuka kurejea kwenye matumizi ya dawa za kulevya” ameongeza Waziri Jenista.
Vilevile ameeleza kuwa, serikali imeweka jitihada kubwa katika kuzuia matumizi ya dawa za kulevya nchini kwa kuimarisha elimu na mikakati ya kukabiliana na tatizo hili kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, semina, makongamano, mikutano, vilabu vya kupinga rushwa na dawa za kulevya shuleni na vyuoni.
Ameendelea kueleza kwamba, mwaka 2023, Serikali ilianzisha kituo maalumu cha Habari na Mawasiliano (Call Centre) kilichopo makao makuu ya ofisi za DCEA ambapo wananchi wanaweza kupiga simu namba 119 bila malipo na kutoa taarifa za wahalifu wa dawa za kulevya au kupata elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya.
Katika kupanua wigo wa udhibiti dawa za kulevya nchini, Serikali imefungua ofisi mpya tano za Mamlaka katika ngazi ya kanda ambazo ni nyanda za juu kusini ambayo ofisi zake ziko Mkoa wa Mbeya inahudumia mikoa ya Mbeya, Songwe, Katavi, Rukwa Njombe na Iringa; Kaskazini ambayo ofisi zake ziko Mkoa wa Arusha inahudumia mikoa ya Arusha, Manyara Kilimanjaro na Tanga.
Pwani Yenye ofisi katika Mkoa wa Mtwara, inahudumia Mikoa ya Pwani, Mtwara, Lindi, Ruvuma na Morogoro; Kanda ya ziwa ambayo ofisi zake ziko Mkoani Mwanza inahudumia Mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Simiyu na Shinyanga, pamoja na Kanda ya kati yenye ofisi Mkoani Dodoma inahudumia Mikoa ya Dodoma, Kigoma Singida na Tabora.
Pamoja na mafanikio hayo bado serikali imeendelea kuwekeza katika udhibiti wa dawa za kulevya ambapo mwaka 2023 imenunua boti yenye kasi (Speed Boat) itakayotumika kufanya doria baharini kukabiliana na uingizaji wa dawa za kulevya kama vile heroin na methamphetamine.