Scolastica Msewa, Bagamoyo – Pwani.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS wamewataka Wavunaji wa Mazao ya Misitu kuvuna ndani ya maeneo waliyopewa vibali, ili Taifa liwe na misitu endelevu na Serikali iingize mapato.
Akizungumza katika kikao cha Wadau wa Mazao ya Misitu Kanda ya Mashariki na Kaskazini inayojumuisha Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro mjini Bagamoyo Pwani, Kaimu Kamanda wa Kanda ya Mashariki, PCO. Mathew Ntilicha amesema mvunaji anapopewa kibali azingatie mipaka yake ya uvunaji.
Amesema, “mnapopewa kibali cha uvunaji, mzingatie uvunaji wako usivuke eneo la uvunaji wako kwani usipovuna sawa na kibali chako malengo yaliyowekwa na serikali tunashindwa kuyafikia, sisi TFS tuna jukumu la kulinda rasilimali ya taifa katika misitu ikiwa ni pamoja na kukaa na wadau na kuwaelekeza na kusaidia sehemu enye changamoto ili malengo ya serikali yatimie.”
Ntichila ambaye alikuwa akiongea kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za misitu Tanzania TFS, Prof. Dos Santos Silayo TFS Kanda ya Mashariki amesema wameona wafanye kikao na wadau wa mazao ya misitu ili kukumbushana kanuni, sheria na taratibu za uvunaji wa mazao ya misitu.
Naye Mhifadhi Mkuu wa TFS, Yusuph Kajia amewataka Wafanyabiashara wa mazao ya misitu katika kanda hiyo, kufuata kanuni, sheria na taratibu za uvunaji na usafirishaji ili wafanye biashara iliyo halali.
Kwa upande wake Mjasiriamali wa mkaa, Eva Kaaya amewataka wafanyabiashara wenzake kuwa waadilifu wa kulipia kama serikali inavyotaka.