Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU, Mkoa wa Manyara, Suzan Raymond ametoa rai kwa Wananchi kujiandaa vyema kwa kutofanya makosa ya kuchagua Viongozi wasiofaa wakati wa kipindi cha uchaguzi wa Serikali za Mtaa.
Suzan ameyasema hii leo Mei 17, 2024 katika mafunzo na Waandishi wa Habari yaliyoandaliwa na TAKUKURU Mkoa wa Manyara, yaliyolenga kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya mapambano dhidi ya rushwa wakati wa uchaguzi.
Amesema, Wanahabari wana nafasi kubwa ya kuhabarisha umma juu ya athari za rushwa, jambo ambalo litasaidia Wananchi kupata uelewa wa namna ya kuchagua Viongozi bora, ambao watalinda na kutetea maslahi ya jimbo na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mwanasheria wa TAKUKURU, Martin Makini amewataka Waandishi hao kuwa mtari wa mbele kutoa elimu juu ya rushwa na uchaguzi na kwamba faini ya kosa hilo ni shilingi milioni moja au kifungo cha miaka mitatu jela kwa mgombea pamoja na mpiga kura atakayebainika kutenda kosa la kutoa na kupokea rushwa.