Wananchi wametakiwa kuhakikisha wanaibeba ajenda ya Nishati Safi ya kupikia kwa vitendo, ili kuunga mkono jithada za Serikali katika kulinda mazingira dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameyasema hayo katika Kijiji cha Msomera Wilaya ya Handeni  Mkoani Tanga, wakati wa hafla ya kugawa mitungi ya gesi na majiko banifu 1500 ikiwa ni mwendelezo wa juhudi za Wizara za kugawa nishati safi ya kupikia na kuunga mkono jitihada za Rais kufikisha asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.

Amesema, ‘ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ni ya Mhe.Rais mwenyewe na ndio kinara hivyo lazima tumuunge mkono kwa vitendo kwa kuacha kukata miti kwa ajili ya kupikia.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Wakili Albert Msando amesifu jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha watanzania wote wanatumia nishati safi ya kupikia na kuwataka Wsnanchi kutumia vema fursa ya majiko banifu na mitungi ya gesi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Renatus Nkwabi amesema nishati safi ya kupikia ni kwa ajili ya watanzania wote na ndio maana REA imetoa majiko banifu kuunga mkono juhudi za Serikali juu ya ajenda ya nishati safi ya kupikia.

Jumla ya Kaya zaidi ya 3,000 za wilaya ya Msomera zimepatiwa majiko banifu na mitungi ya gesi kuwezesha Wananchi waliohamia Msomera kunufaika na nishati safi ya kupikia.

Mshindi Parimatch Kitaa Cup 2024 kupata zawadi nono
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Mei 18, 2024