Scolastica Msewa, Chalinze – Pwani.
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha kupoza Umeme cha Chalinze mkoani Pwani ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 93.7.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Kilumbe Ngenda wakati Kamati ikikagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi huo wa Kituo cha kupoza Umeme cha Chalinze
Alisema Kamati hiyo imefurahishwa na hatua za Maendeleo ya ujenzi wa mradi huo iliyofikiwa baada ya kukagua hatua zote ikiwa ni pamoja na eneo la mitambo ya kupokea Umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Nyerere na eneo la mitambo ya kupoza umeme, transfoma sita zilizofungwa na kazi ndogo ndogo zinazoendelea kukamilisha ujenzi huo.
“Niwapongeze kwani kazi iliyofanyika ni kubwa sana kutoka asilimia 55 tuliyoikuta awamu iliyopita na Sasa mradi umefikia asilimia 93.7 ambapo pia Kuna baadhi ya majengo yamekamilika kwa asilimia 100 mfano ni jengo la kuendeshea mitambo na kusema kukamilika kwa ujenzi wa mradi huo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM chama ambacho kimekuwa kikiahidi na kutekeleza ahadi zake kwa wananchi,” alisema.
Naye Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema, “nataka tuihakikishie kamati na Mheshimiwa spika wa bunge kwamba maelekezo ya kamati na mapendekezo yote tunayapokea kwa weledi mkubwa sana na kuhakikisha tunafanyia kazi ili kuhakikisha miradi hii yenye tija kubwa sana kwa taifa inaendelea kutekelezeka vizuri.”
Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya Meneja wa Mradi Newton Livingstone alisema Mkandarasi anaendelea na Kazi za ujenzi wa miundombinu ya Kituo hicho ikiwa ni pamoja na Barabara, nyumba za Wafanyakazi na ghala la kuhifadhia mitambo ambapo kazi hizo haziathiri uendeshaji wa Kituo hicho.
Alisema tayari ujenzi wa miundombinu wezeshi ili kusafirisha na kupoza Umeme unaotoka Bwawa la Mwalimu Julias Kambarage Nyerere la Rufiji kuja Chalinze umekamilika na megawati 235 zinaingia kwenye gridi ya Taifa kupitia Kituo hicho na kufanikiwa kumaliza mgao wa Umeme nchini.
Afisa uhusiano huduma kwa wateja TANESCO Mkoa wa Pwani, Esta Msaki amewataka wananchi katika maeneo mradi huo ulikopita waendelee kulinda na kutunza miundombinu ya mradi huo ili iwe endelevu kwani wapo ambao huaribu miundombinu kwa makusudi na wengine kwa kutokujua.
“Huu mradi serikali imewekeza kwa asilimia 100 kutoka pesa za watanzania hivyo ni mradi wa watanzania hivyo tuendelee kutunza na kulinda miundombinu yetu ili tuendelee kupata umeme wa uhakika,” alisema Esta.