Mlinda Lango wa Manchester United Andre Onana anasema anahitaji kutwaa Ubingwa wa Kombe la FA, kwa ajili ya mashabiki wa klabu hiyo.

Manchester United itashuka Dimbani mwishoni mwa juma hili (Jumamosi – Mei 25) katika mchezo wa Fainali ya Kombe la FA utakaowakutanisha na Mabingwa mara nne mfululizo wa England Manchester City.

Onana ambaye bado kiwango chake hakijakubalika tangu alipotua klabuni hapo mwanzoni mwa msimu huu 2023/24, amesema ushindi dhidi ya Manchester City ambao utawapa Ubingwa wa FA, utatosha kuwapoza Mashabiki wao.

Amesema Manchester United imekuwa na safari ndufu ya kusaka mafanikio msimu huu, na tayari wametoka kapa katika michuano yote waliyoshiriki, hivyo kilichobaki kwa sasa ni kuhakikisha wanapambana na kuambulia ubingwa wa Kombe la FA.

Onana amesema: “Lazima tuendelee kufanya kazi kwa bidii, tuendelee kuhimizana sisi kwa sisi ili kupata kitu kwa ajili ya Mashabiki wetu. Mchezo wa Fainali dhidi ya Manchester City una umuhimu mkubwa sana kwetu, tunapaswa kushinda ili kurudisha furaha kwa Mashabiki wetu.

“Kurejea kwa baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi kama Lisandro Martinez ni ishara nzuri kwetu ya kuhakikisha tunapambana siku hiyo. Waliopona wote wana umuhimu katika kikosi chetu, kwa hiyo tutahakikisha tunapambana uwanjani.

“Waliorejea kikosini wameanza kufanya mazoezi, kwa hiyo tutegemee mazuri kutoka kwao kwenye mchezo wa Jumamosi, kwa sababu tunahitaji kila mtu, tunahitaji wachezaji wetu wote, tunawahitaji mashabiki wetu kwa sababu itakuwa mechi ngumu sana.

“Umekuwa msimu mgumu kwangu kwa sababu hadi sasa hakuna tulichofanikiwa, lakini ukiniuliza nini ninachokihitaji kwa sasa, nitakujibu kutwaa taji la FA ambalo litakuwa maalum kwa Mashabiki wetu. Wanapaswa kuwa pamoja na sisi, nasi tutapambana hadi mwisho.”

Wiki ya AZAKI: FCS, Vodacom Foundation wasaini makubaliano
Mwanza: Zaidi ya Watumishi 150 washiriki mafunzo mfumo wa NeST