Hadija Bagasha – Tanga.
Shirika la THPS kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani kupitia kituo cha kudhibiti na kuzuia Magonjwa cha U.S CDC’ wamekabidhi mtambo wa kupima kiwango cha matumizi ya Dawa Kinga kwa waraibu wa Dawa za kulevya ‘METHADONE’, katika Kliniki yakutolea huduma kwa Waraibu wa Dawa za kulevya Mkoa wa Tanga, ‘MAT-BOMBO’.
Akikabidhi kifaa hicho kwa niaba ya Shirika hilo Mkurugenzi Mashirika huduma za Kinga kutoka THPS, Dkt. Appolinary Bukuku amesema Mashine hiyo imegharimu Dola 31,500 sawa na Shilingi 82,000,000.
Amesema, “mradi wa Afya Hatua unashirikiana na vituo 101 vya Huduma za Afya, kuhakikisha vina mahitaji yote muhimu ikiwemo watumishi wa Afya na kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi mkubwa,kwa upekee katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga-Bombo ,tumebahatika kutoa huduma kwa Waraibu wa Dawa za kulevya ili kuboresha na ubora wa maisha yao.
Bukuku amesema kliniki ya waraibu wa Dawa za kulevya katika Hospitali ya Rufani ‘MAT-BOMBO’ inahudumia waraibu wa Dawa za kulevya 683 kila siku na waraibu 1094 wamesajiliwa tokea kuanzishwa kwa kliniki hiyo, hivyo wameona kazi ya kupima Dawa kwa mikono imekuwa ikiwafanya watumie muda mrefu sana wa kutoa huduma za Dawa.
“THPS baada ya kuiona hiyo changamoto tulipoanza kufanya kazi Tanga tulilazimika Kuahishirisha shughuli zingine ili tufanikishe jambo hili,pia THPS kupitia Mradi wa Afya Hatua itaendelea kulipia Dola 2000, kwaajili ya leseni ya mfumo wa ufanyaji kazi wa kifaa hicho kila mwaka” Amesisitiza Dkt.Bukuku
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Tanga, Dkt. Imani Clemence aliwashukuru wadau hao kwa msaada huo nakwamba utasaidia kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa Waraibu wa Dawa za kulevya.
“Tunawashukuru sana THPS pamoja na mpango wa wa dharura wa Rais wa Marekani wa kupambana na UKIMWI ( PERFAR), kupitia kituo cha Marekani cha kudhibiti na kuzuia Magonjwa cha U.S CDC, umechangia sana kuboresha huduma za Afya kwa Wananchi wa Tanzania, hivyo tunawashukuru sana kwa msaada wenu na tunaomba muendelee kutoa msaada zaidi kwakuwa bado mahitaji ni mengi sana katika Sekta hii ya Afya,” amesisitiza Dkt.Clemence.