Hamida Kamchalla – Tanga.
Sababu ya kuongezeka kwa waraibu wa dawa za kulevya katika Mkoa wa Tanga imetajwa kuwa ni kutokana na Mkoa huo kuwa mpakani, hivyo kuwa na njia za panya za kupenyeza dawa hizo na wasafirishaji kulipwa ujira mkubwa, ili kufanikisha biashara husika jambo ambalo linaongeza watumiaji.
Kaimu Kamishna wa Kinga na Tiba, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Dkt. Casian Nyandindi ameyasema hayo kwenye mkutano wa wadau wa huduma za waraibu (MAT), Mkoa wa Tanga na kuongeza kuwa wanapaswa kutoa elimu ya kutosha kwa jamii juu ya madhara ya dawa hizo.
Amesema, “Dawa hizi zinachangia Kwa kiasi kikubwa kuleta tatizo la afya ya akili, lakini pia wapo wenye tatizo hili ambayo wanakwenda kutumia dawa za kulevya, tusikate tamaa kuwaelimisha wale ambayo bado hawajazidiwa ukimsaidia mraibu umesaidia jamii nzima.”
Dkt. Nyandindi amebainisha kuwa matumizi ya dawa za kulevya ni mtambuka hivyo kila mmoja anapaswa kuwajibika kwa kufuata taratibu, kanuni na sheria katika kutimiza wajibu wake, huku Daktari wa magonjwa ya akili, ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Dawa za Methadone, Warles Karata akisema Mkoa umepata athari kubwa kutokana na ongezeko la matumizi ya dawa hizo.
“Serikali imeona waraibu waliopo waweze na kupatiwa dawa, na wale ambayo wameitika na kuanza dawa wanaendelea vizuri na maisha wakiwa na familia zao, tuna Asas za kiraia ambazo zinapambana na waraibu katika mitaa yao, lakini bado tunahitaji Taasisi mbalimbali ziweze kuliona hili na kuweza kuwa msaada kwa hawa waraibu,” amesema.
Naye Meneja wa Wadau wa huduma za Waraibu (MAT) Mkoa wa Tanga, Dkt. Otmar Massawa amesema wamejipanga kuhakikisha wanaongeza jitihada katika kushuhulikia kwa ufanisi matumizi mabaya ya dawa za kulevya huku akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mpango huo tangu kuanzishwa kwake na kusema wapokea huduma 1,113 walijiandikisha na 683 wanaendelea na huduma.
Kwa upande wa waraibu wanaopokea huduma wametoa ushuhuda kuhusu maisha yao ya uraibu na jinsi MAT ilivyowasaidia kurudi katika maisha yao ya kawaida, huku mkutano huo ukiwezeshwa na Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) chini ya mradi wa Afya Hatua unaofadhiliwa na Mpango wa Dharura wa Rais wa nchi ya Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR), kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (U.S. CDC).