Kiungo Mshambuliaji wa kutoka nchini Burkina Faso Stephen Aziz Ki ametuliza hali ya hewa ndani ya Young Africans, baada ya kusema bado ana imani na Rais wa Klabu Hersi Said.
Aziz Ki amezua sintofahamu klabuni hapo, kufuatia mkataba wake wa sasa kutarajia kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu 2023/24, huku akiwa hajasaini mkataba mpya hadi sasa.
Kiungo huyo aliyesajiliwa Young Africans mismu uliopita akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast amesema licha ya kuwa na ofa kadhaa, bado anaipa nafasi kubwa klabu hiyo ya Jangwani, kutokana na ukaribu uliopo kati yake na Rais Hersi Said.
Aziz Ki amesema suala kubwa ambalo Rais wa Klabu amekuwa akimsisitiza ni kusalia klabuni hapo, ili kutimiza ndoto za Young Africans za kucheza Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kama walivyofanya katika Kombe la Shirikisho msimu uliopirta 2022/23.
“Mpaka sasa Mimi ni Mchezaji wa Young Africans na nafasi kubwa zaidi nawapa Young Africans, namwamini Rais wa Klabu yeye ndie amenileta hapa, tuna makubaliano yetu mimi na yeye kuwa Young Africans inapaswa kucheza fainali ya Afrika na tutwae kikombe, hiyo ndio ndoto yangu,”
“Ikitokea tumecheza Fainali na kubeba ubingwa nitamfuata Rais kumwomba baraka zake ili niondoke zangu, ila kwasasa bado malengo yangu na Young Africans hayajatimia mpaka tucheze Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika” amesema Aziz Ki
Mbali na mafanikio ya kutwaa Ubingwa msimu huu 2023/24, Aziz Ki pia anawania Tuzo ya Ufungaji Bora akichuana na Kiungo wa Azam FC Feisal Salum ‘Fei Toto’ kila mmoja akifunga mabao 18 hadi sasa.