Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Juma Ramadhan Mgunda ametangaza vita kubwa dhidi ya JKT Tanzania, ambao wataamua hatma ya kikosi chake msimu huu 2023/24.

Simba SC ina mtihani wa kumaliza katika nafasi ya Pili iliyokaliwa na Azam FC kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, huku klabu hizo kutoka jijini Dar es salaam zikilingana alama, zote zikiwa na alama 66.

Kocha Mgunda ametangaza vita hiyo akiwa katika Mkutano na Waandishi wa Habari mapame leo Jumatatu (Mei 27), alipozungumzia maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo huo wa mwisho wa Ligi Kuu msimu huu.

Kocha huyo amesema: Ni mechi ya kufunga shule, kwa maana ligi ya msimu huu tunakwenda kuimaliza, maandalizi yetu yapo vizuri na tunafahamu umuhimu wa mchezo wetu wa kesho dhidi ya JKT Tanzania.

Tunahitaji matokeo katika mchezo huu ili kufahamu tutamaliza vipi Ligi ya Msimu huu. Siku zote ninaamini haya ni mashindano na JKT Tanzania ni washindani wenzetu, kwa hiyo tumejiandaa vizuri kwenda kushindana na washindani wenzetu.

Ni mchezo wenye maamuzi, na mchezo wowote wenye kuhitaji maamuzi inategemea na mahitaji yanayohitajika, kila mmoja ana mahitaji yake, sisi kama Simba SC tuna mahitaji yetu kwenye mchezo huu na wenzetu wana mahitaji yao. Kwa hiyo ninaamini utakuwa mchezo wenye ushindani mkubwa ambao mwisho wa yote unatakiwa kutoa maamuzi.

Kisaikolojia wachezaji wangu wanafahamu umuhimu wa mchezo huu, siku zote huwezi kumnenepesha Ng’ombe kwenye mnada kwa hiyo vitu vyote tumeshavizungumza na tumeshavifanyia kazi, kwa hiyo kisaikolojia wachezaji wangu wapo vizuri na wanajua umuhimu wa mchezo wetu wa kesho. Sisi kama Simba SC tumejiandaa vizuri kuelekea kwenye mchezo huo kuhakikisha kwamba licha ya kufanya vizuri mwisho wa siku tunapata matokeo yaliyokuwa mazuri.

Ikumbukwe kuwa Mshindi wa Kwanza na wapili katika msimamo wa Ligi Kuu wataiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku Mshindi watatu na wanne wakishiriki Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Al Ahly, Zamalek wamkosha Hossam Hassan
JKT waichokonoa Simba SC