Josephine Majula, WF – Kagera.
Polisi Wilayani Missenyi wametakiwa kuwa mabalozi kwa wananchi wanaowazunguka ili kuwafikishia elimu ya masuala ya fedha waliyoipata kutoka kwa Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha iliyoko katika kampeni ya kutoa elimu ya fedha kwa umma katika mikoa mbalimbali nchini.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Missenyi, SP. Jonas Sira Soa wakati akizungumza na Askari Polisi katika semina iliyofanyika katika Viwanja vya Kituo Cha Polisi Kyaka, Wilaya ya Missenyi, mkoani Kagera.
Amesema, “tunaahidi kuwaelimisha Polisi wengine ambao hawajapata elimu hii, lakini pia tutawajengea uwezo Polisi Jamii ili wawaelimisha wananchi ambao wapo karibu nao ili waepukanane na mikopo umiza.”
Soa ameongeza kuwa, elimu ikiwafikia wananchi wote nchini itaisaidia Serikali kupondokana na kupunguza migogoro ya kesi mbalimbali zinazoendelea kwenye Vituo vya Polisi kuhusu mikopo inayowakumba wananchi mbalimbali.
Naye Mkaguzi wa Polisi, Baraka Mafwimbo, aliiomba Serikali kuongeza nguvu ya kudhibiti na kuimarisha mifumo ya Taasisi zinazohusika na utunzaji wa taarifa binafsi za wananchi kuhakikisha zinalinda taarifa hizo ili kuepusha taarifa hizo kufikiwa na watoa huduma ya mikopo na kuweza kuwashawishi kukopa fedha.
“Binafsi nimewahi kupigiwa simu na kushawishiwa kuchukua mkopo na watoa huduma ambao sikujua taarifa zangu wamezitoa wapi, lakini walikuwa wananielezea kama wananifahamu lakini hawakuweza kufanikiwa kwa kuwa nimewahi kupata elimu ya masuala ya fedha zamani,” alisema.
Kwa upande wake Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Mary Mihigo, aliwasisitiza wananchi na polisi kuhakikisha wanatumia kuomba mikopo kwenye Taasisi za Fedha zilizosajiliwa rasmi ili kujiepusha na matapeli.
Alisema, “utajua kuwa ni Taasisi rasmi ya kukopesha, kupitia Tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambayo imeorodhesha Taasisi rasmi zote za utoaji mikopo nchini hivyo ni lazima mwananchi kabla hajakopa kujiridhisha kwenye usajili wa Taasisi husika.”
Aidha, alisema Serikali kupitia Wizara ya Fedha, itaendelea kutoa elimu ya masuala fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa mpana wa masuala ya fedha ikiwemo elimu ya mikataba, uwekezaji na mikopo umiza.