Sintofahamu ya wapi atakapocheza Beki wa Kushoto wa Chelsea Ian Maatsen imeibuka, huku akiwa katika maandalizi ya mwisho ya kucheza Mchezo wa Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya akiwa na Borussia Dortmund anayoitumikia kwa mkopo.
Borussia Dortmund ya Ujerumani itapapatuana na Miamba ya Soka kutoka mjini Madrid-Hispania mwishoni mwa juma hili katika Uwanja wa Wembley nchini England, ili kumaliza ubishi wa nani atakuwa Bingwa wa Barani Ulaya upande wa vilabu msimu huu 2023/24.
Sintofahamu ya Maatsen imeibuliwa na Gazeti la Daily Mail, ambalo limeandika kuwa Beki huyo wa Kushoto kutoka nchini Uholanzi bado hajaamua ni wapi anataka kucheza msimu ujao 2024/25.
Gazeti hilo limeripoti: “Ian Maatsen bado hajaamua juu ya mustakabali wake na Klabu ya Chelsea licha ya kusaini mkataba wa hadi Januari 2026, huku Borussia Dortmund ikiwa na nia ya kuendelea kumtumia kwa kumsajili moja kwa moja, ikitarajia kumia kipengele cha mkataba wake, ambacho kinaruhusu Beki huyo kuuzwa kwa Pauni Milioni 35.”
“Maatsen, ambaye ni zao la akademi ya Chelsea, kwa sasa yuko Dortmund kwa mkopo. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 alianza mchezo mmoja pekee wa Ligi Kuu mwanzoni mwa msimu huu, kabla ya kutimkia Ujerumani Januari 2024, ambako amekuwa akianza mara kwa mara na kucheza kila dakika ya mechi zao za mtoano za Ligi ya Mabingwa.
“Hata hivyo Kocha mpya wa Chelsea Enzo Maresca anatazamwa kama suluhisho la Maatsen kurudi klabuni hapo ama kusalia jumla Dortmund. Hata hivyo Chelsea haina changamoto ya Beki wa kushoto, kwani kwa sasa inao Marc Cucurella na Ben Chilwell.”