Naibu Waziri wa Maji wa Tanzania, Mhandisi Kundo Andrea Mathew amesema wamekamilisha MoU itakayowezesha ushirikino wa nchi tatu za Malawi, Tanzania na Msumbiji, ili kuanzisha na kuendesha Kamisheni ya Bonde la Ruvuma, ambapo Tanzania itafaidika zaidi kwa vile makao makuu yatakuwa Manispaa ya Mtwara – Mikindani na hivyo kutoa ajira kwa nafasi za kada za chini.
Mhandisi Kundo ambaye yuko Nchini Angola kumwakilisha, Jumaa Aweso katika Mkutano wa 42 wa Mawaziri wa Nishati na Maji wa SADC, amesema MoU hiyo inatarajia kuwekwa saini Jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa Mwezi Julai, 2024, kkwa kushirikisha nchi wanachama wa Bonde la Ruvu na wafadhili, ambao ni GIZ, GWP na IUCN.
Amesema, “tumeandaa mradi utakaowezesha Usimamizi wa Pamoja/Shirikishi wa Rasilimali za Maji katika Bonde la Mto Ruvuma wenye thamani ya Dola Millioni Saba (7) ambao utafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani (Global Environment Facility – GEF).”
Kupitia ushirikiano huo, wameandaa mradi utakaowezesha Usimamizi wa Pamoja/Shirikishi wa Rasilimali za Maji katika Bonde la Mto Ruvuma wenye thamani ya Dola Millioni Saba (7) ambao utafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani (Global Environment Facility – GEF).
Mkutano wa 42 wa Kamati ya Mawaziri wa Nishati na Maji wa SADC umepitisha jumla ya kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 1.46 kwa ajili ya maandalizi ya mradi huo ambao unatekelezwa kwa Awamu ya Pili sasa ambapo katika Awamu ya Kwanza pamoja na kujenga uwezo wa wataalamu, mradi uliwezesha kuchimba visima vitano (5) vya uchunguzi katika mwamba maji (aquifer) wa Kimbiji na Mpera.
“Mwamba maji huu ni chanzo muhimu cha maji kwa Jiji ya Dar es Salaam. Visima vya uchunguzi vinawezesha kupatikama kwa takwimu ambazo zinatumika katika kuwezesha usimamizi endelevu wa mwamba maji husika na rasilimali za maji kwa ujumla,” amesema Naibu Waziri Mhandisi Kundo.
Aidha, Awamu ya Pili ya Mradi huu inatekelezwa katika Jiji la Dodoma ambalo kwa sehemu kubwa hutegemea maji chini ya ardhi kwani katika eneo la Nzuguni kuna mwamba na maji yamegunduliwa miaka ya karibuni, hivyo kutachimbwa visima 3 ambapo visima 2 vitakuwa ni vya uchunguzi na kingine ni cha uzalishaji.
Hata hivyo amesema, “itafanyika taftishi ya kubaini maeneo ambayo maji ya mvua hivilia chini ya ardhi (recharge areas) ili kuweza kuyalinda na kuyatunza dhidi ya uhalibifu. Jumla ya Dola 125 za Kimarekani zitatumika katika mradi huu,” amesisistiza Naibu Waziri.