Boniface Gideon – Tanga.
Chuo cha Ubaharia cha Dar es Salaam Maritime Institute – DMI, kimewataka Vijana kuchangamkia fursa za masomo ya Ubaharia ili kuingia kwenye soko la ajira kwa wakati,hii inatokana na kada hiyo ya Ubaharia kuwa na fursa nyingi za ajira ndani na nje ya Nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Usafirishaji majini ambaye pia ni Mhadhiri kutoka DMI, Kapteni Mohamed Kauli wakati wa maadhimisho ya wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayofanyika mkoani Tanga katika viwanja vya Popatilal, kuwa fursa za ajira katika Sekta za usafirishaji majini ni nyingi katika soko la ajira ndani na nje, hivyo ni vyema Vijana wakachangamkia masomo ya Ubaharia.
Amesema, “Chuo chetu kinatoa Elimu na Ujuzi katika Sekta za usafirishaji majini,tunawandaa wahitimu kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu kuwa watumishi bora katika Sekta ya Majini, lakini pia tunawatafutia ajira ndani na nje ya Nchi katika Mataifa ambayo tunafanya nao kazi, kwasasa hakuna janja janja za kuingia kwenye Sekta za Ubaharia kama zamani.
Kwa upande wake Mwanafunzi wa chuo hicho, Masaka Julius ambaye amebuni Mtambo wa Roboti kwa ajili ya kubeba mizigo viwandani ,alisema kwakupitia mafunzo mbalimbali waliyoyapata wanauwezo wakwenda kujiajiri wenyewe,
“Kupitia mafunzo tuliyapata chuoni na kama mnavyoona hapa tumeweza kubuni mitambo mbalimbali ambayo inasaidia katika shughuli za kila siku, hususani viwandani,hivyo tukitoka chuoni tuna uhakika wa ajira hasa kwakujiari”Alisema