Heldina Mwingira.

Takwimu zinaonesha kuwa, zaidi ya mtu mmoja kati ya watano wamepitia unyanyasaji wa kingono kazini ambapo Wanawake ndiyo huathirika zaidi na unyanyasaji wa kingono ikilinganishwa na wanaume hali ambayo hutokana na mamilioni ya Wafanyakazi wa kike kulazimika kufanya kazi katika mazingira magumu, chuki au kufedhehesha na kupata aina mbalimbali za unyanyasaji wa ngono usiokubalika.

Wengi wao huombwa rushwa ya ngono, hufanyiwa utani usiostahili na mguso wa kimwili bila ridhaa yao ambao huashiria unyanyasaji na unyanyasaji wa namna hii, huhusishwa na utashi wa mtu binafsi, umri au thamani, kwa mfano mnyanyasaji anaweza kuwa na mamlaka kiutendaji, mmiliki wa ofisi na hupelekea kuwa sababu ya mtu anayenyanyaswa na hata wakati mwingine hutokea kwa watu wenye cheo kimoja.

Sababu.

Unyanyasaji wa aina yoyote huwa una sababu na ndiyo maana Dar24 Media ililazimika kuzungumza na baadhi ya Wanawake (majina yao yamehifadhiwa), ambao walisema, “ukatili wa kingono mara nyingi husababishwa na muathirika kuhitaji fursa ya kupandishwa cheo/ kupata kazi/ kuendelea kufanya kazi na ili aweze kufanikiwa bosi huonesha msimamo kwamba bila ngono mwanamke hawezi kupata fursa hiyo husika.”

Mwingine alisema, “wakati mwingine ni matamanio ya kimwili tu yaani tamaa kwamba bosi anamuhitaji binti kimahusiano na kumjengea ugumu katika kazi zake kama vile kumpa vikwazo kiutendaji ili amkubali kimapenzi, hali ambayo huleta ugumu wa uwajibikaji na hata wengine kufukuzwa kazi.”

“Wanawake makazini tuna shida sana kwa kweli maana nilikuwa nafanya kazi ofisi fulani msimamizi wa ile ofisi alikuwa ananitaka kimapenzi ananishika maumbile yangu na ukimkataza na anakujibu ni vitu vya kawaida na kuniambia mimi ni mtu mzima jambo gani nisilolijua katika dunia hii,’ alisema mmoja wao.

Kwa upande wao wasimamizi na Wakuu wa Taasisi tofauti, nao walipata wasaa wa kuzungumzia uhalisia wa suala hili la unyanyasaji wa kingono, wakionesha kutokuwa tayari kukiri wala kuzungumzia iwapo unyanyasaji huo unafanyika katika ofisi wanazozifanyia kazi wakisema hawajawahi kusikia.

Ni wazi kwa majibu hayo yanaendelea kuthibitisha kuwa unyanyasaji wa kingono kazini bado ni kitu cha usiri, hivyo kuonesha ipo haja ya kuweka jitihada na nguvu za ziada katika kupata ukweli wa mambo.

Viashiria.

Vitu hatarishi ambavyo vinaweza kusababisha kuwa na unyanyasaji wa kingono kazini, ni pamoja na uwepo wa asilimia kubwa ya jinsia ya kiume wenye mamlaka katika taasisi zao, unywaji wa pombe katika matukio ya kijamii ofisini unaoweza kupelekea mtu kushindwa kujizuia, urasimu na kutochukulia hatua za haraka kwa Wafanyakazi wenye tabia mbaya.

Hata hivyo, si Wanaume pekee wanaopaswa kulaumiwa katika suala hili, kwani baadhi ya Wanawake hufikiri kwamba wanapaswa kuonekana watu wanaotamanika, wenye mvuto wa kimapenzi na kukubalika hivyo kudhani kwamba huo ndiyo msingi wao wa ulaghai na kupelekea wakati mwingine ushawishi wa kingono mahali pa kazi.

Athari.

Unyanyasaji wa kingono kazini, huathiri Wanawake zaidi ambao unaweza kusababisha mtu au watu kupoteza kazi zao kwa sababu ya kuogopa jambo hilo, pia wenye mamlaka wanatakiwa kuzingatia suala la uaminifu usio egemea upande wowote wa muhusika kwani unaweza kusababisha uharibifu mkubwa wa kisaikolojia na kupungua ama kupoteza kabisa umakini.

Aidha, hali hiyo inaweza pia kujenga hofu na kupelekea madhara ya afya ya akili husababisha kuchukua likizo ya ugonjwa au mbaya zaidi wanalazimika kuacha kazi zao, huku Wanawake wengi wakiona kama alama mbaya kwao, ambayo inadhoofisha hali yao kujiamini na kiutendaji hivyo pia ufanisi wao kikazi hupungua.

Hata hivyo, jambo hili pia wakati mwingine huathiri hata kesho yao mfano pale mwathirilka aliyeacha kazi anapohitaji udhamini kutoka kwa waajiri wao wa awali, au kutoa sababu za kuacha kazi ya awali hivyo kuweza kuwa na ugumu katika kupata fursa nyingine kwa kukosa ushirikiano kwa mwajiri wa mwanzo.

Suluhisho.

Kutokana na ufinyu wa fursa na uhaba wa ajira ikiwemo unyanyasaji wa kingono makazini, hali hii huongezeka siku baada ya siku, lakini pia inawezekana kupunguza ama kuondoa kabisa changamoto hii kwa kufanyika vitu vifuatavyo sehemu zote za kufanyia kazi kuwe na sera za zinazohusu unyanyasaji wa kingono.

Wasimamizi na wafanyakazi wote wa kiume na wa kike, lazima wafahamu kuhusu unyanyasaji wa kingono na jinsi ya kushughulikia suala hilo, kwani ikiwa sera ipo na iko wazi ni rahisi mtu anayenyanyaswa na anayefikiria kufanya unyanyasaji atajua haki za mtu huyo ni nini hivyo atakuwa muoga na kupunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa unyanyasaji.

Pia, yawepo mafunzo maalum ambayo yatasaidia Wanawake kukabiliana na wanyanyasaji wa namna hivyo na hivyo wao na jamii nzima kwa ujumla ya makazini kuwa salama na zipo sheria, mikataba, kanuni sera na miongozo ambayo hukataza aina yoyote ya unyanyasaji wa kimapenzi katika maeneo ya kazi na hata pia katika mazingira mengine yoyote.

Juni 2019, Wanachama Shirika la Kazi Duniani – ILO, walipitisha mkataba wa msingi unaojulikana kama Mkataba wa Unyanyasaji na Unyanyasaji (C190). Mkataba huo ni wa kwanza kuweka viwango vya kisheria vya kimataifa vya kuzuia na kukabiliana na unyanyasaji katika ulimwengu wa kazi ambayo ilianza kutumika kisheria chini ya sheria za kimataifa.

Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya 2004, imeweka wazi masuala ya unyanyasaji wa kimapenzi kuwa aina ya ubaguzi, imeukataza na imetoa hukumu ya faini isiyozidi shilingi milioni tano kwa yeyote atakayekutwa na hatia juu ya jambo hilo.

Aidha, Sheria ya Matoleo Maalum ya Makosa ya Kimapenzi ya 1998 inaadhibu pia unyanyasaji wa kimapenzi na zifuatazo zinachukuliwa kama aina ya tabia zinazojumuishwa katika unyanyasaji wa kimapenzi, (i) kusababisha usumbufu wa kimapenzi kwa mtu (ii), kusema neno lolote (iii), kutoa sauti au ishara yoyote au kuonyesha kitu chochote ikiwa ni pamoja na kiungo chochote iwe cha kike au cha kiume au ishara hiyo kuonwa na Mwanamke.

Maoni.

Licha ya unyanyasaji wa kingono kusumbua Wanawake wengi makazini, bado matukio kama hayo hayaripotiwi mara kwa mara kwasababu ya hofu ya kutoaminiwa, kulaumiwa, kulipizwa kisasi kijamii au kitaaluma na kushushwa hadhi kijamii.

Hali hii, hupelekea ugumu katika kuondoka kwa changamoto kama hizo kwani hutendeka katika mazingira ya faragha na hivyo tunaamini kuwa uelewa juu ya tatizo na njia za kukabiliana nayo, itasaidia kupunguza kiwango chake kwa kiasi kikubwa.

Vile vile Wanawake, Wafanyakazi na Wataalamu wa taaluma mbalimbali ni lazima wachukue hatua na kuhakikisha ofisi zao zinakuwa salama na zisizo na vitendo vya unyanyasaji wa kingono.

Mashirika ya ndege ya Kimataifa kutangaza utalii wa Tanzania
Royar tour yaendelea kuinufaisha Sekta ya Utalii