Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amesema Mashirika ya ndege ya Kimataifa ya Qatar Airways, Emirates na Turkish Airlines yataanza kutangaza vivutio vya utalii vivavyopatikana nchini Tanzania.
Kairuki ameyasema hayo wakati akielezea vipaumbele vya wizara alipokuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Leo Jijinu Dodoma, ambapo amesema wizara itaendelea kutangaza utalii ndani na nje ya Nchi kupitia matangazo katika Ligi na Mashindano ya Michezo yenye wafuatiliaji wengi zaidi Duniani.
Amesema, “tutatumia watu mashuhuri na wenye ushawishi, Mabalozi wa hiari wa utalii, vyombo vya habari vya Kimataifa vyenye ushawishi pamoja na mitandao ya kimataifa ya utalii kama vile TripAdvisor na Expedia Group, vyombo vya habari kama CNN.”
Kairuki ameongezea kuwa, Wizara inaendelea kukamilisha taratibu za kujitangaza kupitia Ligi za Michezo mikubwa Duniani za Marekani na Uingereza na Matukio makubwa ya Burudani ambapo Wizara itaweka mifumo maalum ya mawasiliano katika misitu ya hifadhi ya asili na mashamba ya miti, ili kubaini matukio ya moto na kutoa elimu ya uhifadhi.
Aidha ameongeza kuwa, “katika kuelekea mkutano wa wadau wa Nyuki Kimataifa mwaka 2027 Wizara itaanza utekelezaji wa Programu ya Nyuki kwa Vijana na Wanawake ili kuandaa wataalamu na wajasilisamali wa mazao yatokanayo na asali na mazao mengine ya nyuki.”
Wizara kwa mwaka ujao wa fedha itapunguza Ada ya Leseni ya Biashara za utalii kwa wakala wa kupandisha watalii mlimani (mountain climbing), kufuta tozo kwa waongoza watalii wenye leseni hai kila wanapoingia hifadhini.
“Wadau watalipa Ada ya Leseni ya Biashara za utalii kwa kutumia shilingi ya Tanzania badala ya Dola za Marekani pamoja na kuongeza muda wa Leseni ya Biashara za utalii kwa Waongoza watalii ambapo kwa sasa itadumu kwa kipindi cha miaka mitatu badala ya mwaka mmoja wa sasa,” amesema.