Serikali Nchini, imesema ipo imara na inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kwa lengo la kuwaletea Wananchi maendeleo, hivyo waendelee kuipa ushirikiano.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wananchi katika Mji Mdogo wa Katoro, Geita na kudai kuwa utekelezaji wa miradi hiyo utawawezesha Wananchi kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kushiriki katika shughuli za kujiingizia kipato.
Amesema, “Serikali yenu inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ili kuwawezesha wananchi wake kufanya shughuli za kimaendeleo. Miradi hii ni ile ya huduma za kijamii ambayo Watanzania, Wanakatoro kila siku lazima iwaguse. Serikali imejikita hapo.”
Waziri Mkuu amesema kwasasa Serikali itaongeza fedha kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa madarasa ili kuwezesha idadi ya vyumba vya madarasa viendane na idadi ya Wanafunzi na kuwa na uwiano mzuri, ili kupunguza msongamano madarasani.