Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewataka Watanzania kudumisha amani, mshikamano na upendo na kamwe wasigawanywe kwa sababu yoyote.
Amesema hayo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ibada ya kuwekwa wakfu Askofu Robert Yondam Pangani wa Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo la Kusini Magharibi iliyofanyika leo Juni 2, 2024 katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji mkoani Mbeya.
Amesema, “Waumini wenzangu huyu si malaika ni binadamu itafika wakati atachoka naomba mumtie moyo, na msiache kumuombea na kumtii inawezekana kuna anayejua kuliko yeye lakini yeye amepewa fursa ya kuwaongoza nyinyi hivyo mumtii. Pia tusibaguane kwa dini zetu au vyama vyetu vya siasa, sisi tuliokaa hapa hatujatambuana kwa makabila yetu tunatambuana kwa utanzania wetu, wakati wote muhubiri amani na mtu yeyote mwenye shida aone Tanzania ni mahali salama.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema Rais Samia ameunganisha taasisi za dini na alichangia milioni 50 katika Kanisa la Moravian kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mkoani Dodoma.
Naye, Askofu Robert Yondam Pangani amesema kuwa amepokea kwa heshima na kwa unyenyekevu nafasi aliyopewa na anaahidi kuungana na viongozi wa dini kuhakikisha amani inadumu pamoja na kuimarisha ushirikiano na Serikali.