Huenda kuna baadhi ya watu hawajui kwamba zamani za kale kulikuwa na michezo ya Kiafrika iliyokuwa na umaarufu na heshima kubwa hata kabla ya kuwasili kwa michezo kama vile Mpira wa Miguu, Mpira wa Mikapu Mpira wa Nyavu na mingineyo, ambayo kwa masikitiko michezo hii iliachwa na kusahaulika polepole hapa barani Afrika.
Muda mrefu kabla ya ukoloni, mchezo wa kuruka juu ulikuwa wa Kimataifa ambao uliwapa umaarufu Wanyarwanda kwani walifanya vyema huku ukiwa ni utamaduni wenye umuhimu mkubwa katika jamii ya Wanyarwanda, kwani Wanaume mara nyingi walikuwa wakiruka zaidi ya futi 6 na inchi 6 katika maonesho ya uwezo wao wa kimwili.
Katika sherehe muhimu, Wafalme wa Rwanda waliamuru mfululizo wa shughuli za kitamaduni kufanyika na kuruka juu ilikuwa moja ya shughuli iliyojumuishwa kwenye hafla kama hizo na hata ilifanywa pia katika harusi muhimu na nje ya Mahakama kwenye mikusanyiko ya ndani ya umuhimu.
Vijana na wazee pia walicheza mchezo uliofahamika kama ‘gusimbuka urukiramende’ ambapo Watoto wangepanda vijiti viwili, kuweka nguzo nyingine kwa usawa, na kushindana kulingana na umri wao, halafu Watoto wanaochunga mifugo walitumia muda wao wa mapumziko kucheza mchezo huo, hadi jioni ambapo wangerudisha ng’ombe Nyumbani.
Hivyo unapozungumzia michezo mingi ya asili, huu wa kuruka juu huwezi kuuacha na pia ukumbuke ipo mingi ambayo imesahaulika ikiwemo kuruka chini, kuruka kamba, kombolela kwa watoto, kula mbakishie baba, danadana, kurusha tiara, tobo ngimu nk, ambayo kwa kiasi fulani ilisaidia kuamsha ubongo na kufanya uwe na uwezo wa ziada wa kufikiri mambo.