Gideon Gregory, Dodoma.

Serikali imesema inaendelea na uwekezaji wa ujenzi wa mabomba ya kusafirisha na kusambaza gesi majumbani ambapo kwa kushirikiana na Sekta Binafsi, ina mpango wa kuongeza miundombinu ili kupokea meli kubwa za gesi ya LPG na hivyo kushusha gharama za bidhaa hiyo.

Kauli hiyo, imetolewa hii leo Juni 3, 2024 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Neema Lugangira aliyetaka kujua kama Serikali haioni haja ya kupunguza gharama ya gesi ili lengo la kufikia asilimia 80 ya Watanzania kutumia Nishati safi ya kupikia ifikapo 2033/34.

Amesema, “Serikali inaendelea kuhamasisha Sekta Binafsi zinazojihusisha na usambazaji na uuzaji wa gesi ya LPG na gesi asilia pamoja na kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya kujaza gesi vinavyohamishika na visivyohamishika kwa kila Wilaya.”

Aidha, ameongeza kuwa Serikali inafanya jitihada kuhakikisha bei ya Nishati safi ya kupikia inapungua ambapo kwa upande wa mitungi ya Gesi inayopatikana kutoka kwenye viwanda vya kusafisha mafuta (LPG – Liquified Petroleum Gas), ruzuku imetolewa kwa mitungi 83,500 yenye thamani ya shilingi Bilioni 3.5.

Rais Samia atunukiwa udaktari wa Falsafa wa heshima
MALIMWENGU: Mruko zaidi ya futi sita kabla