Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uvuvi katika maeneo mbalimbali kwa kujenga miradi ya masoko ya samaki yatakayowawezesha wananchi kufanya biashara zao kwa ufanisi na kukuza uchumi.
Majaliwa ameyasema hayo hii leo Juni 3, 2024 baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mwalo wa kupokelea samaki na soko la kisasa la samaki Chato Beach akiwa katika ziara ya siku moja wilayani Chato, Geita na kudai kuwa Serikali inaimarisha na kuwashirikisha wavuvi na wafugaji katika mipango ya maendeleo yao.
Amesema,”mradi huu unaotoa fursa kwa yeyote aliyeanza na anayetaka kujikita kwenye sekta ya uvuvi kunufaika na kujiongezea kipato. Kitendo cha Serikali kuleta soko hili hapa ni kuhakikisha wanasogeza fursa kwa wavuvi wa eneo hili, soko hili ni lenu, imarisheni uchumi wenu kupitia soko hili.”
Awali, Meneja wa Mradi Mhandisi George Kwandu alisema kukamilika kwa mradi huo kutapunguza upotevu wa samaki hususan dagaa baada ya kuvunwa, pia utaongeza thamani ya mazao ya uvuvi na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali unaotarajiwa kukamilika Agosti 2, 2024.