Taasisi za Umma zimetakiwa kufanya tathmini za awali ya hali ya utekelezaji wa mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini katika taasisi zao na kuwasilisha katika Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu kabla ya tarehe 15 Julai, 2024.
Maagizo hayo yametolewa leo Juni 3, 2024 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera ,Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama wakati wa hafla ya Uzinduzi wa nyaraka za msingi za Ufuatiliaji na Tathmini nchini na utiaji sahihi mikataba ya makubaliano katika kuimarisha shughuli za Ufuatiliaji na Tathmini nchini.
Waziri Mhagama amesema kuzinduliwa kwa mwongozo huo utasaidia kuongeza ufanisi katika Ufuatiliaji wa Tathmini na kuhimiza matumizi ya matokeo ya tathmini hizo katika kufanya maamuzi na kuboresha utekelezaji na utendaji katika ngazi zote.
“Katika kutekeleza mwongozo huu, ninaelekeza Taasisi za Umma kuandaa taarifa ya utekelezaji wa Tathmini zote zilizofanyika kwa mwaka wa fedha 2023/24 na zinazotarajiwa kufanyika kwa mwaka wa fedha 2024/25 ili Ofisi yangu iweze kuandaa Mpango wa Tathmini wa mwaka 2024/25 na kufuatilia utekelezaji wake,” amesema Mhagama
Aidha katika kutekeleza mwongozo huo Mhagama ameelekeza yafuatayo :-Kufanya Tathmini ya Awali ya hali ya utekelezaji wa Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini katika Taasisi zao (M&E Readiness Assement), Kuandaa Mwongozo wa Matumizi (Operational Manual) ambao unaeleza utekelezaji wa Ufuatiliaji na Tathmini wa kila siku katika taasisi zao. Mwongozo huo uoneshe namna ambavyo vitengo, idara au sehemu za U&T zitakavyofanya kazi kwa kuzingatia Mwongozo huu.
Maelekezo mengine ni pamoja na Kuandaa Mpango wa Ufuatiliaji (Monitoring Plan) kwa kuonesha maeneo na kazi zote zitakazofuatiliwa kila siku kulingana na Mpango Kazi wa Taasisi (Action Plan) na mipango ya utekelezaji wa afua mbalimbali, Kuandaa Mpango wa Tathmini (Evaluation Plan) kwa kuonesha tathmini za afua za maendeleo zitakazofanyika katika kipindi husika.
Sambamaba na hayo ameelekeza Kuandaliwa kwa moduli za utendaji zinazojumuisha viashiria muhimu vya kupima utendaji wa Taasisi,Kuteua wataalamu (U&T Champions) kutoka Idara na Vitengo vyote vya taasisi husika. Wataalamu hao watashirikiana na Idara/Kitengo cha U&T katika utekelezaji wa Mwongozo huu.
Pia amewasisitiza Makatibu Wakuu, Watendaji Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Wakurugenzi wa Vitengo vya U$T katika Taasisi zote za Umma kuendelea kuimarisha Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini vilivyoanzishwa kwa kutengewa bajeti ya kutosha kutekeleza shughuli zake na kuwajengea uwezo wa kitaalamu watumishi waliopo katika vitengo hivyo na kuhakikisha taasisi za umma zinafanya tathmini za mara kwa mara za utekelezaji wa Sera, Mipango, Miradi na Programu mbalimbali za Serikali na kuwasilisha taarifa hizo Ofisi ya Waziri Mkuu.
Awali, akitoa neno la utangulizi Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amefafanua miongozo iliyozinduliwa kuwa ni Jumuishi wa Ufuatiliaji na Tathmini unalenga kuziongoza taasisi za umma kuhusu namna ya kutekeleza majukumu ya Ufuatiliaji na Tathmini. Mwongozo huu umeainisha hatua za kufuata katika ufuatiliaji, ufanyaji wa Tathmini, maandalizi ya viashiria na kupima utendaji wa shughuli za Serikali.
Pia umezinduliwa Mwongozo wa Tathmini ya utayari wa Taasisi za Umma katika kutekeleza shughuli za Ufuatiliaji na Tathmini umelenga kutathmini uwezo, udhaifu, fursa na changamoto zinazokabili taasisi za umma katika kutekeleza shughuli za ufuatiliaji na tathmini na hivyo kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha.
Aidha Mwongozo mwingine ni Mwongozo Kitaifa wa Tathmini (National Evaluation Guideline) unalenga kutoa namna bora ya kuratibu na kusimamia tathmini nchini. Kimsingi mwongozo huu unalenga kuhakikisha mipango ya tathmini inafuatwa, matokeo ya tathmini yanatumika na utamadumi wa kufanya tathmini unajengwa.
Dkt. Yonazi amesema utekelezaji wa miongozo hiyo kwa kiasi kikubwa unategemea uwepo wa Mfumo Jumuishi wa Kielektroniki wa Ufuatiliaji na Tathmini (Government wide integrated M&E System)
“Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Serikali Mtandao, ipo katika mchakato wa maandalizi ya Mfumo huo. Kukamilika kwa mfumo huo kutasaidia katika ukusanyaji, uchakataji na utoaji wa taarifa za Ufuatiliaji na Tathmini kwa wakati (real time data) na pia kuwezesha upimaji utendaji kazi utakaochangia katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi,” alieleza Dkt. Yonazi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa uzinduzi huo huku akieleza kuwa hatua hii ni jambo zuri na kukumbusha kuwapa nafasi wataalamu wa masuala ya ufuatiliaji na tathmnini ili kuyafikia matarajio ya Tanzania ya sasa na ya baadae.
Naye Kadari Singo Mkuu wa Taasisi ya Uongozi amesema upo umuhimu wa kuendelea kusimamia vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini katika Wizara na Taasisi zetu ili kusaidia kuleta matokeo yanayokusudiwa na kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu ya kila siku.
“Ni vyema kukawa na desturi ya kufanya tathmini kuanzia mtu mmoja mmoja, nafasi ya familia, jamii na katika maeneo yetu ya kazi hii iwe ni sehemu ya maisha ya kila mmoja na kusadia kujua wapi unaenda sawa na wapi urekebishe na kuepuka kuenenda bila malengo,” alieleza Singo
Aliongezea kuwa, ili kuendelea kuwa na matokeo katika utendaji kazi wa kila siku, jamii haina budi kubadili mtazamo na kuyapa umuhimu mkubwa masuala ya tathmini na ufuatiliaji kama nyenzo ya kujipa nafasi ya kufanya vizuri zaidi kuliko ambapo isingefanyika.