Serikali Nchini, imepongezwa na Benki ya Dunia – WB, kwa kuwa ni miongoni mwa Mataifa yanayoongoza kwa kuwadambazia umeme Wananchi wake.
Akitoa pongezi hizo leo Juni 4, 2024 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini, Nathan Belete amesema kuwa Benki hiyo inatambua kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Tanzania.
Amesema, “hapa Afrika, Tanzania ni mfano mzuri katika usambazaji wa Nishati ya Umeme kwa wananchi. Tumejipanga kuwa na mazungumzo zaidi na kuona namna bora zaidi ya kusaidia katika masuala ya nishati safi ya kupikia kwa kufadhili na kuhusisha sekta binafsi kwa kuangalia fursa zilizopo.”
Belete ameongexa kuwa, Benki hiyo inafadhili pia mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400 ukutoka Iringa hadi Sumbawanga na kuunganisha nchi za Tanzania na Zambia.
Amesema, Benki ya Dunia itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuiendeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia ambayo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kinara wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumzia pongezi hizo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameishukuru Benki ya Dunia kwa pongezi hizo na kusema kuwa Benki hiyo ni mdau mkubwa wa maendeleo nchini na kuwa wamekuwa na ajenda ya kushirikiana katika miradi ya nishati.
Amesema, “tumefurahi kusikia nchi yetu imepiga hatua na tumejipanga kuendeleza miradi mingine ya nishati ili kuhakikisha kuna utoshelevu wa Nishati hiyo nchini.”
Aidha, Dkt. Biteko ameongeza kuwa, “tutaendelea kushirikiana na Benki ya Dunia na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza kila fedha tunayopata lazima iwe na thamani kwa wananchi. Wizara pamoja na Shirika letu la umeme TANESCO limepongezwa kwa kushughulikia vizuri suala la nishati nchini, hata hivyo ni lazima kuangalia mbali zaidi si tu kuridhika kwa hapa tulipofika.”