Umoja wa Afrika (AU) na Shirika la Kilimo na Chakula (FAO) wamemtambua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, kama vinara wa kuwapambania wavuvi wadogo Afrika, ikiwa ni mwendelezo wa Mkutano wa Kimataifa wa wavuvi wadogo uliofanyika kwa siku mbili, Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo umeshirikisha watu zaidi ya 1000 kutoka mataifa mbalimbali Barani Afrika, ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Naibu Waziri Mkuu, Dotto Biteko akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kushuhudia hoja mbalimbali zikijadiliwa kwa lengo la kuwaendeleza wavuvi wadogo nchini Tanzania.

Akizungumza katika Mkutano huo wa kwanza Barani Afrika mwakilishi wa umoja wa Mataifa AU-IBAR, Hellen Moepi-Guebama, alisema mkutano huu wa kwanza uliohusisha wavuvi wadogo na kushirikisha watu wa kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, una lengo la kuangalia namna nzuri ya kuwakomboa wavuvi wadogo Afrika.

“Tunatambua mchango wa Rais Samia kuanzisha na kusaidia wavuvi wadogo haswa kwa namna ya kutafsiri sera, miongozo, kanuni, pamoja na mpango kazi wenye lengo la kuisaidia sekta hii muhimu ya uvuvi barani Afrika.

“Aidha Tanzania kwa kupitia jitihada za Rais Samia, tumeshuhudia mkutano mkubwa wa wavuvi wadogo wenye lengo la kukusanya maoni ya wavuvi yatakayokwenda kufanyiwa kazi katika Mkutano wa Kimataifa utakaofuata nchini Italia,” alisema Hellen.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Kilimo na Chakula FAO, nchini Tanzania, Dkt. Tipo Nyabenyi Tipo, alisema kufanyika kwa mafanikio kwa tukio la wavuvi wadogo ni juhudi madhubuti na malengo ya juu aliyokuwa nayo Rais Samia.

“Nchini Italia mwaka jana Waziri Ulega aliahidi Tanzania kuandaa mkutano huu, ambao leo tunaona umefanikiwa kwa asilimia kubwa. Haya ni matunda ya serikali ya Rais Samia ambapo tunaona ni mwendo mzuri katika sekta hii ya uvuvi mdogo,”alisema Dkt. Tipo.

Nyabenyi alisema endapo sekta ya uvuvi mdogo itaendelezwa na kupewa ushirikiano, jamii itanufaika kwa sababu sekta hiyo inatumika pia kama chanzo cha mapato cha watu wengi.

Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, aliwashukuru wadau wote kwa kushiriki mkutano huo, huku akisema kuwa kama Tanzania ina dhamira ya kuwainua wavuvi wadogo kwa kuhakikisha kuwa inafanyia kazi changamoto mbalimbali zinazowakabili ili sekta hiyo iwe na manufaa kwa wote, akisisitiza kuwa sekta ya uvuvi mdogo inahusisha asilimia 95 ya uvuvi wote nchini.

Katika Mkutano huo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, maoni yanayotolewa na wadau yataenda kufanyiwa kazi katika Mkutano wa Kimataifa wa Uvuvi huko nchini Italia.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Juni 8, 2024
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Juni 6, 2024