Lydia Mollel – Morogoro.

Ubovu wa barabara inayotoka Lukobe Mwisho kuelekea Mazimbu jirani na Barabara kuu ya Morogoro – Dodoma, umekuwa kero kwa wakazi wa kata Lukobe eneo la Lukobe juu Manisapaa ya Morogoro, hali ambayo imepelekea kupanda kwa gharama za maisha hasa upande wa usafiri na Maji na kuwalazimu Wananchi kufunga njia, ili kufikisha ujumbe kwa Serikali.

Wakizungumza na Dar24 Media Wananchi hao wamesema hakuna barabara inayofika katika Kata yao, kwani iliyokuwepo awali imefungwa kupisha ujenzi wa njia ya Treni ya Mwendokasi na kupelekea kubuni njia mbadala katika eneo la shule jambo ambalo limepelekea wao kukusanyika na kufungua njia hiyo kwani inaleta usumbufu kwa Wanafunzi.

Wamesema, licha ya uharibifu wa barabara lakini hakuna upatikanaji wa maji Safi na salama na kwamba wananunua dumu moja kwa shilingi 800.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi – CCM Wilaya ya Morogoro mjini, Fikiri Juma akiongozana na viongozi mbalimbali wa Serikali, ametembelea eneo hilo na kumuelekeza Meneja wa TARURA Wilaya ya Morogoro kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo, pamoja na kuwataka LATRA kurejesha huduma ya usafiri.

Mohamed Mwanda, ni Meneja wa TARURA ambaye amesema amepokea maagizo hayo na kuhaidi utekelezaji wa haraka, ili Wananchi wa eneo hilo wapate huduma ya Barabara kwa wakati.

Miundombinu bora ni msingi wa maendeleo endelevu na kuboresha maisha ya Wananchi kwani hufanya usafiri kuwa rahisi na haraka, hivyo kuimarisha uhusiano wa kijamii na kiuchumi.

Dkt. Biteko: Wazazi wapelekeni Watoto shule
TURACO: Vijana changamkieni fursa za Utalii