Swaum Katambo, Mpanda – Katavi.

Wakati Serikali ikiweka juhudi kuboresha miundombinu ya shule ili Wanafunzi wapate elimu katika mazingira mazuri, baadhi ya Watu wasio waaminifu wameng’oa madirisha 10 ya aluminiam katika shule ya Msingi Kasisiwe, iliyopo Kata ya Ilembo Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi.

Watu hao wanaodhaniwa kuwa ni wezi, wametenda tukio hilo usiku wa kuamkia Juni 6, 2024, kabla ya kukurupushwa na raia wema waliosababisha watu hao kuyatelekeza na kutokomea kusikojulikana wakati wakifanya juhudi za kuyahamisha madirisha hayo.

Sehemu ya Madirisha yaliyovunjwa na kutelekezwa.

Mkuu wa shule ya msingi Kasisiwe, Jane Sigaleti amekiambia chanzo hiki kuwa thamani ya madirisha yaliyovunjwa ni Shilingi 3,100,000 ambapo kwa sasa wamejipanga kuchukua hatua za awali kwa kuweka mlizi atakayekuwa akilinda miundombinu ya shule hiyo.

Naye Diwani wa Kata ya Ilembo, Joseph Kang’ombe amelaani kitendo hicho na kusema sicha kiungwana, kwa kuwa shule hiyo ndiyo inayotegemewa na wakazi wa maeneo hayo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kasisiwe, Jane Sigaleti.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mapinduzi, Jovin Kitundu amesema baada ya kupata taarifa walifanya juhudi za kuwataarifu Jeshi la Polisi ambapo baada ya kufika eneo la tukio wezi hao walikimbia na kutelekeza madirisa hayo chini.

Kwa upande wao baadhibya Wananchi wa Kata hiyo wamelaani tukio hilo kwa kudai kuwa linawarudisha nyuma kimaendeleo huku wakiomba ofisi ya Mkurugenzi Manispaa ya Mpanda kusaidia suala la ulinzi katika shule hiyo.

Diwani wa Kata ya Ilembo, Joseph Kang’ombe.

Imebainika kuwa asilimia kubwa ya shule hazina walinzi jambo linalohatarisa usalama wa miundombinu ya shule.

 

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Juni 9, 2024
Malabe: Uchangiaji wa damu hauna madhara kiafya